KIKOSI cha Azam FC leo Jumanne asubuhi kimejifua kwa mara ya kwanza kikiwa kambini jijini Ndola, Zambia.
Azam FC imeweka kambi ya takribani siku 12 nchini humo, ikiwa inajiandaa na msimu huu unaotarajia kuanza kutimua vumbi Septemba mwaka huu.
Programu ya Kocha Mkuu wa Azam FC, George Lwandamina, inaonyesha kuwa mara baada ya mazoezi hayo ya asubuhi, kikosi hicho kitapumzika na kuendelea na sehemu ya pili ya mazoezi leo jioni.

Wakati kikianza mazoezi ya kwanza, kikosi hicho kinatarajia kucheza mchezo wa kwanza wa kirafiki dhidi ya timu ya Red Arrows, utakaofanyika Uwanja wa Levy Mwanawasa, kesho Jumatano saa 9.00 Alasiri (sawa na saa 10.00 jioni Tanzania).
Mechi hiyo itakuwa inamrudisha nyumbani, kiungo mkabaji wetu mpya, Paul Katema, ambaye atakuwa akicheza dhidi ya timu yake ya zamani, tuliyomnunua akitokea huko.
Kocha Mkuu wa Azam FC, George Lwandamina ‘Chicken’, anatarajia kuutumia mchezo huo kama sehemu ya kuwaangalia wachezaji wake namna wanavyoendelea kupokea programu yake ya maandalizi ya msimu mpya.

Mbali na mchezo huo, kikosi hicho kitacheza mechi nyingine tatu za kirafiki za kimataifa na timu za huku, zingine zikiwa ni dhidi ya Kabwe Warriors (Agosti 29), Forest Rangers (Septemba 02) na mabingwa wa Zambia, Zesco United (Septemba 03).