MSHAMBULIAJI wa Azam FC, Prince Dube, ameshatua jijini Ndola, Zambia akiwa tayari kabisa kujiunga na wenzake mazoezini kujiandaa na msimu huu unaotarajia kuanza Septemba mwaka huu.

Dube ambaye ndiye mfungaji bora wa Azam FC msimu uliopita akifunga jumla ya mabao 17 kwenye mashindano yote na kutoa pasi tano za mwisho, alikuwa mapumzikoni kwa wiki nne akiuguza majeraha ya misuli ya paja.

Nyota huyo ametua Zambia saa 6.30 mchana (sawa na 7.30 mchana kwa saa Tanzania), akitokea nchini kwao Zimbabwe, ambapo muda wowote kuanzia sasa ataanza rasmi mazoezi na wenzake tayari kujiweka sawa kabisa kuelekea msimu huu.

Mshambuliaji, Prince Dube, akiwa amepokelewa na Meneja wa Azam FC, Luckson Kakolaki na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano, Thabith Zakaria ‘Zaka Za Kazi’

Aidha mshambuliaji huyo, ametua na kuonyesha tabasamu akimaanisha amefurahia vilivyo kurejea tena kazini kwenye timu bora ambayo imekuwa ikilipeperusha vema jina lake hadi kupelekea kuitwa mara kwa mara katika timu ya Taifa ya Zimbabwe.

Mshambuliaji amepokelewa vema na Meneja wa timu, Luckson Kakolaki, aliyeambatana na Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam FC, Thabith Zakaria ‘Zaka Za Kazi’.