KIKOSI cha Azam FC tayari kimewasili jijini Ndola, Zambia leo Jumatatu asubuhi tayari kumalizia maandalizi ya msimu huu unaotarajia kuanza mwezi ujao.

Azam FC imetua Zambia kwa ndege ya Shirika la Kenya (KQ), ikianzia safari jijini Dar es Salaam na kupitia Kenya kabla ya kuunganisha ndege ya kutua Ndola, Zambia.

Msafara wa Azam FC umehusisha wachezaji wote iliyowasijili kwa ajili ya msimu huu, isipokuwa wachezaji saba walioitwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kipa Wilbol Maseke, mabeki Edward Manyama, Lusajo Mwaikenda, viungo Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Wengine waliobakia kambini na Taifa Stars, ni viungo washambuliaji, Idd Seleman ‘Nado’ na Ayoub Lyanga, huku nahodha Agrey Moris, akibakia jijini Dar es Salaam baada ya kupata majeraha akiwa mazoezini juzi.

Wachezaji na Maofisa wa timu ya Azam FC wakiwa tayari wamekanyaga ardhi ya jijini Ndola, Zambia.

Mshambuliaji Prince Dube, aliyekuwa amepewa mapumziko maalum wiki nne wakati akiuguza majeraha, anatarajia kujiunga na kikosini keshokutwa Jumatano, akitokea nchini kwao Zimbabwe.

Mara baada ya kikosi cha Azam FC kutua Zambia, kilipewa mapumziko ya siku moja, na kinatarajia kuendelea na programu ya mazoezi kesho Jumanne asubuhi na jioni kikiwa chini ya Kocha Mkuu, George Lwandamina na Msaidizi wake, Vivier Bahati.

Kikiwa kambini Ndola, kikosi cha Azam FC kitacheza mechi nne za kirafiki na timu za huku, kitaanza mchezo wa kwanza, Agosti 25 kwa kumenyana na Red Arrows, kitaumana na Kabwe Warriors Agosti 29, kabla ya kukipiga na Forest Rangers Septemba 02, huku kikihitimisha kambi kwa kuwavaa mabingwa wa nchi hiyo, Zesco United.