KIKOSI cha Azam FC kinatarajia kuelekea jijini Ndola, Zambia, keshokutwa Jumatatu kuweka kambi ya takribani siku 12 kwa ajili ya kumalizia maandalizi ya msimu huu 2021-2022 unaotarajia kuanza mwezi ujao.

Azam FC itaenda nchini humo ikiwa na kikosi chake chote kitakachocheza msimu ujao, akiwemo mshambuliaji Prince Dube, ambaye anatarajia kujiunga na timu moja kwa moja nchini Zambia akitokea nchini kwao Zimbabwe.

Akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam FC, Thabith Zakaria ‘Zaka Za Kazi’, alisema kuwa kikosi hicho kikiwa kambini Zambia, kitacheza mechi nne za kujipima nguvu na timu za huko kabla ya kurejea nchini Septemba 4, mwaka huu.

“Baada ya kambi ya takribani wiki mbili na nusu kwenye uwanja wetu wa Azam Complex, Azam FC inatarajia kuondoka nchini Jumatatu ya tarehe 23 (keshokutwa) kuelekea Ndola, Zambia kwa ajili ya mwendelezo wa kambi (maandalizi ya msimu huu),” alisema.

Kikosi cha Azam FC, kikiendelea na maandalizi ya msimu huu kwenye makao makuu yake, Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Zaka Za Kazi, alizitaja mechi za kirafiki ambazo kikosi hicho kitacheza kikiwa humo, ambapo itaanza kwa kukipiga dhidi ya Red Arrows (Agosti 25), mechi ya pili itaumana na vigogo wa huko Zanaco (Agosti 29), itapepetuana na Forest Rangers Septemba 02 kabla ya kuhitimisha kambi hiyo maandalizi Septemba 03 kwa kuwavaa mabingwa wa nchini hiyo, Zesco United.

Aliongeza kuwa; “Tutakuwa kule kwa takribani wiki moja na nusu na tutarejea Dar es Salaam (Septemba 4) tayari kabisa kwa mchezo wetu wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika kwa ajili ya msimu wa 2021/2022.”

Azam FC tumepangwa kuanza na Horseed ya Somalia kwenye raundi ya awali ya michuano hiyo mikubwa namba mbili barani Afrika, mchezo wa kwanza ukifanyika Uwanja wa Azam Complex kati ya Septemba 10-12 huku wa marudiano ukipigwa ugenini, kati ya Septemba 17 hadi 19 mwaka huu.

Aidha mshambuliaji Prince Dube, ambaye bado hajaungana na timu kwa ajili ya maandalizi ya msimu huu, anatarajia kujumuika na wenzake kambini Agosti 25 mwaka huu, baada ya kumaliza mapumziko ya wiki nne aliyopewa wakati alipoenda kufanyiwa matibabu nchini Afrika Kusini.

“Baada ya matibabu aliyofanyiwa kule Afrika Kusini alipewa mapumziko ya wiki nne, zitakazokamilika Agosti 24 na tarehe 25 atakuwa kambini pale nchini Zambia kuungana na wenzake kwa ajili ya kumalizia sehemu ya maandalizi ya msimu ili tukirudi hapa tuwe kamili ya kikosi chote,” alisema.