KLABU ya Azam imethibitisha kuwa haitafanya tamasha lake la Azam FC Festival kwa msimu huu kutokana na muda wa maandalizi ya msimu mpya kubana.

Azam FC kwa mara ya kwanza iliweza kuanzisha tamasha hilo mwaka jana, lililofanyika na kupokelewa kwa furaha na mashabiki wa soka nchini huku klabu hiyo ikinufaika na mauzo ya jezi pamoja na kuiuza vema nembo yake kwa maelfu ya mashabiki waliojitokeza.

Akiongea na mtandao rasmi wa klabu, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam FC, Thabith Zakaria ‘Zaka Za Kazi’, alisema kuwa muda umekuwa ni mchache sana wa maandalizi kutokana na msimu uliomalizika kuchelewa kuisha.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Azam FC, Thabith Zakaria ‘Zaka Za Kazi’, akithibitisha kutokuwepo kwa Azam FC Festival.

“Timu yetu ilianza kambi tarehe 14 ya mwezi huu (Agosti) na imekuwa ikifanya mazoezi magumu moja kwa moja isingewezekana kufanya tamasha hili katika wiki ya kwanza ambayo ni leo tarehe 21 au 22 kwa sababu bado timu ipo kwenye mazoezi makali na ingekuwa tunakatisha mazoezi kwa mujibu wa programu ya mwalimu,” alisema.

Aliongeza kuwa wiki ijayo kikosi hicho kitakuwa nchini Zambia kwenye mwendelezo wa kambi kwa ajili ya kuiweka timu sawasawa, huku akidokeza kuwa baada ya kurejea nchini wachezaji wengi wataenda kwenye majukumu ya timu zao za Taifa, hivyo ingekuwa ni ngumu kuwapata wachezaji wao wote kwa ajili ya tamasha hilo.

“Kutokana na ratiba hii ngumu ilivyokuwa majadiliano kati ya benchi la ufundi na uongozi ikaonekana kilicho bora ni kuwaomba radhi mashabiki wetu, kuwaomba radhi wale wote tuliokuwa tukishirikiana nao katika tamasha hili na wale wote waliotarajia tamasha hili kuja kwa sababu imekuwa nje ya uwezo na kwa maslahi mapana ya klabu yetu, tumeona bora mwaka huu tulisitishe,” alisema.

Zaka Za Kazi alimalizia kwa kudokeza kuwa kwa misimu ijayo panapo majaliwa watalifanya kwa ubora zaidi tamasha hilo, ambalo lilifana vilivyo msimu uliopita.