KLABU ya Azam imemtangaza, Dr. Jonas Tiboroha, kuwa Mkurugenzi wa Mpira wa timu hii.

Zoezi la utambulisho wake limefanyika leo Jumatatu mchana kwenye ofisi za timu hii zilizopo Mzizima, Banda la Ngozi, jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa utambulisho, Afisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’, alisema hiko ni cheo kipya ndani ya timu hii, huku akiyataja majukumu yake kuwa ni kusimamia maendeleo yote ya mpira ndani ya Azam FC.

“Kwa uzoefu wake na kuwa kwake kwenye mpira kwa miaka mingi tunategemea atatusaidia sisi kuitoa klabu yetu hapa ilipofika na kwenda mbele kwa kushirikiana pamoja,” alisema Popat.

Tiboroha ni mmoja wa viongozi wachache nchini waliosomea masuala ya michezo katika viwango vya juu.

Aidha akizungumzia uteuzi wake, Tiboroha ameushukuru uongozi wa Azam kwa kumuamini na kumpa nafasi hiyo huku akiahidi kutimiza yale yaliyomfanya kuwa hapo kwa kushirikiana na viongozi wengine ili kuipa mafanikio zaidi timu hii.