KLABU ya Azam FC inatarajia kushuka dimbani kutupa karata yake ya pili kwenye michuano ya Kombe la Kagame, ikiivaa Messager Ngozi ya Burundi, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Alhamisi saa 10.00 jioni.

Vijana wa Azam FC watakuwa na kazi moja tu, kuhakikisha wanavuna alama zote tatu ili kujihakikishia nafasi ya kusonga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo, kwani ikifanya hivyo itafikisha jumla ya pointi sita.

Azam FC ilijikusanyia pointi tatu za kwanza kwenye mchezo wa kwanza wa Kundi B, ikifanikiwa kuwachapa vigogo wa Uganda KCCA mabao 2-0, yaliyofungwa na Paul Peter, ambaye ndiye kinara wa mabao katika michuano hiyo hadi sasa.

Beki wa kushoto wa Azam FC< Pascal Msindo, akiwatoka wachezaji wa KCCA, wakati timu hizo zilipokutana kwenye mchezo wa kwanza wa michuano ya Kombe la Kagame.

Kocha Msaidizi wa Azam FC, Vivier Bahati, anayekiongoza kikosi hicho kwenye michuano hiyo, amesema kuwa pointi tatu za mchezo huo ni muhimu sana, huku akieleza kuwa amekipanga kikosi chake kufanya vizuri.

“Mechi hazifanani ukiangalia mechi ya kwanza tumeshaiacha ya pili tumeiandaa kivingine ili kupata pointi tatu zingine tukijaaliwa naamini mazoezi tuliyofanya uwanjani yatatupa matokeo mazuri,” alisema Bahati.

Naye nahodha wa kikosi hicho kwenye michuano hiyo, kipa Benedict Haule, amesema kuwa wamejipanga vema kupambana kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo.