KIKOSI cha Azam FC kimeanza vema michuano ya Kombe la Kagame, baada ya kuichapa KCCA ya Uganda mabao 2-0 mchezo uliofanyika Uwanja wa Azam Complex usiku wa jana Jumatatu.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake, kikosi cha Azam FC kikiundwa na wachezaji wengi vijana waliokulia kwenye kituo chetu cha kukuza vipaji.

Wachezaji wanaunda kikosi cha Azam FC kwenye michuano hiyo, ni wale waliotoka kwa mkopo, wengine wakiwa kutoka timu yetu ya vijana (Azam FC U-20) walioungana na wachezaji baadhi kutoka timu kubwa ambao hawakupata muda wa kucheza msimu uliopita.

Mtanange huo ulikuwa ukikumbushia fainali iliyopita ya michuano hiyo, iliyofanyika jijini Kigali, Rwanda mwaka 2019, KCCA ikishinda bao 1-0, hivyo kwa ushindi wa jana Azam FC imeweza kulipa kisasi dhidi ya timu hiyo.

Winga wa Azam FC, Idd Kipagwile, awakiwatoka wachezaji wa KCCA.

Azam FC ilibidi isubiri hadi kipindi cha pili kuweza kujipatia mabao hayo mawili, yaliyofungwa kiustadi na mshambuliaji chipukizi, Paul Peter, ambaye msimu uliopita alikuwa kwa mkopo KMC.

Peter alifunga bao la kwanza dakika ya 46, baada ya kugongeana vema na winga hatari, Idd Kipagwile, na baada ya kupenyezewa pasi ya mwisho aliweza kuwazidi maarifa kipa wa KCCA na mabeki wake kwa kupiga shuti safi la juu lillowashinda kuokoa.

Dakika 17 baadaye, shambulizi lililoanzishwa na beki wa kushoto anayechipukia vizuri, Pascal Msindo, aliyewapiga chenga kwa kasi mabeki watatu wa KCCA na kumwekea pasi safi Peter, aliyegusa mpira mara moja na kufunga kiustadi kwa mguu wake wa kulia.

Kiungo wa Azam FC, Tepsie Evance, akimiliki mpira mbele ya beki wa KCCA, Peter Magambo.

Ushindi huo, unaifanya Azam FC kuongoza Kundi B ikiwa na pointi tatu, huku Messager Ngozi ya Burundi na KMKM ya Zanzibar zikifuatia, zote zikiwa na pointi moja, kufuatia sare yao ya bao 1-1 zilipokutana katika mchezo wa kwanza.

Aidha, keshokutwa Alhamisi kikosi cha Azam FC kitashuka dimbani kucheza mchezo wake wa pili kwenye michuano hiyo ikivaana na Messager, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex saa 11.00 jioni.