AZAM FC tunayofuraha kuwataarifu kuwa tumeingia mkataba wa miaka miwili na golikipa, Ahmed Ali Suleiman ‘Salula’, tuliyemsajili kutoka KMKM ya Zanzibar.

Golikipa huyo mwenye umbo kubwa, amesaini mkataba huo mbele ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin ‘Popat’.

Salula ni mmoja wa makipa hodari, akiwa ndio tegemeo katika timu ya Taifa ya Zanzibar ‘Zanzibar Heroes’, anakuja kuongeza nguvu katika eneo la langoni kwenye timu yetu.

Kipa wetu mpya, Ahmed Ali Suleiman ‘Salula’, akiwa ameshika uzi wa Azam FC sambamba na Ofisa Mtendaji Mkuu, Abdulkarim Amin ‘Popat’.

Huo unakuwa usajili wetu wa saba kuelekea msimu ujao, tukiwa na nia ya dhati ya kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika (CC).

Wachezaji wengine tuliowasajili ni beki wa kushoto, Edward Manyama, kiungo mkabaji, Paul Katema (Zambia), viungo washambuliaji, Charles Zulu (Zambia), Kenneth Muguna (Kenya) na washambuliaji Rodgers Kola (Zambia), Idris Mbombo (DRC).