MABINGWA mara mbili wa Kombe la Kagame (CECAFA Kagame Cup), klabu ya Azam FC inatarajia kutupa karata yake ya kwanza kwenye michuano hiyo ikimenyana na mabingwa watetezi, KCCA ya Uganda

Mchezo huo wa Kundi B utakaokuwa ukikumbushia fainali iliyopita ya michuano hiyo, utafanyika kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam kesho Jumatatu saa 3.00 usiku.

Katika fainali hiyo iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nyamirambo, Kigali, Rwanda, Azam FC iliyokuwa ikiundwa na wachezaji wengi vijana kwenye kikosi chake, ilipoteza kwa kufungwa bao 1-0.

Kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Idd Seleman ‘Nado’, akimtoka mchezaji wa KCCA katika mchezo wao wa mwisho kwenye fainali ya michuano hiyo jijini Kigali, Rwanda 2019.

Kikosi cha Azam FC kimekuwa na maandalizi ya wiki moja kuelekea michuano hiyo mikubwa kwenye Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) na mikongwe barani Afrika, kikiwa chini ya Kocha Msaidizi, Vivier Bahati.

Vivier amewajumuisha kikosini wachezaji wa timu kubwa ambao hawakupata muda wa kucheza msimu uliopita, wachezaji wa Azam FC waliokuwa kwa mkopo na baadhi wa timu ya vijana (Azam FC U-20).

Azam FC itaingia kwenye mchezo huo ikitaka kuanza vema harakati ya kulirejesha kombe hilo ililolitwaa mara mbili mfululizo (2015, 2018) kabla ya kulipoteza mwaka juzi, ikitaka kushinda kipute hicho cha ufunguzi.

Rekodi Azam FC vs KCCA

Kwa mujibu wa historia ya michuano hiyo, Azam FC imekutana mara nne na KCCA, ikishinda mara mbili na kupoteza dhidi yao mara mbili, kukiwa hakuna sare yoyote iliyopatikana.

Rekodi za timu hizo zinastaajabisha kwani, kila aliyeshinda dhidi ya mwenzake kwenye mwaka husika basi ndiye alikwenda kutwaa taji la michuano hiyo.

Wababe hao kutoka Wilaya ya Temeke, walikutana na KCCA kwa mara ya kwanza mwaka 2015, Azam FC ikishinda bao 1-0 kwenye hatua ya makundi kabla ya kuichapa tena kwa ushindi kama huo zilipokutana katika nusu fainali na Azam FC ikatinga fainali na kwenda kutwaa taji hilo ikiichapa Gor Mahia ya Kenya 2-0.

Mwaka 2019, KCCA ikatwaa ubingwa baada ya kuitambia Azam FC kwenye mechi zote mbili, ilipotana hatua ya makundi iliibuka kidedea kwa ushindi 1-0 na zikakutana fainali na Waganda hao wakaibuka kidedea kwa ushindi kama huo.

Mara zote timu hizo zilipokutana, basi mashabiki wa soka wamekuwa wakipata burudani safi ya soka la ushindani na mchezo mkali.