WAKATI michuano ya Kombe la Kagame ikitarajia kuanza kutimua vumbi kuanzia keshokutwa Jumapili hadi Agosti 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam, waandaaji wamepanga ratiba mpya kwa timu shiriki ikiwemo Azam FC.

Ratiba mpya iliyopangwa na waandaaji Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), inaonyesha kuwa Azam FC tumepangwa Kundi sambamba na mabingwa watetezi KCCA ya Uganda, KMKM ya Zanzibar na Messager Ngozi ya Burundi.

Kundi A linahusiha timu za Yanga, Express ya Uganda, Atlabara ya Sudan Kusini na Big Bullets ya Malawi.

Azam FC tutafungua michuano hiyo kwa kuivaa KCCA, mchezo utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumatatu ijayo saa 10.00 jioni, mchezo wetu wa pili tutakipiga dhidi ya Messager Agosti 5 saa 7.00 mchana.

Azam FC ilipokutana mara ya mwisho dhidi ya KCCA, kwenye fainali za mwisho za michuano ya Kombe la Kagame zilizofanyika Kigali, Rwanda.

Aidha tutakamilisha ratiba ya makundi kwa kucheza na KMKM mchezo utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex Agosti 7 mwaka huu saa 10.00 jioni.

Endapo tutamaliza nafasi mbili za juu kwenye kundi letu, tutafuzu kwa hatua ya nusu fainali itakayofanyika Agosti 10 na 11 kabla ya mchezo fainali kufanyika Agosti 14.

Tayari kikosi cha Azam FC kimeshaanza maandalizi kuelekea michuano hiyo, kikiwa chini ya Kocha Msaidizi, Vivier Bahati.

Azam FC tutashiriki michuano hii yenye historia kubwa barani Afrika, tukiwa tumeingia fainali tatu mfululizo zilizopita na kutwaa taji hili mara mbili mfululizo (2015, 2018).

Mwaka 2015, tulipotwaa mara ya kwanza tuliifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0, yaliyofungwa na nyota wetu wa zamani, nahodha John Bocco na Kipre Tchetche, mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Tukarudia historia yetu nzuri ya kutwaa taji bila kupoteza mchezo kwa kucheza fainali ya pili mfululizo na kutetea taji letu mwaka 2018, tukikipiga dhidi ya Simba na kuichapa mabao 2-1, yaliyowekwa kimiani na Nahodha Agrey Moris kwa mkwaju wa adhabu ndogo ya moja kwa moja, kabla ya Shabaan Chilunda kutupia msumari wa pili.

Mwaka juzi tuliingia fainali ya tatu mfululizo kwenye michuano iliyofanyika jijini Kigali, Rwanda kikosi cha Azam FC kikiundwa na wachezaji wengi vijana na kupoteza kwenye fainali kwa kufungwa na mabingwa wa sasa KCCA ya Uganda bao 1-0.

Kikosi cha Azam FC, kilipotinga nusu fainali ya Kombe la Kagame mwaka 2019 baada ya kuichapa TP Mazembe ya Congo DR mabao 2-1.

Aidha Azam FC, kabla ya kutinga fainali iliichapa miamba ya Afrika, TP Mazembe mabao 2-1 kwenye mchezo wa robo fainali na nusu fainali ikaiondoa Maniema kwa mikwaju ya penalti 5-4.