MSHAMBULIAJI hatari wa klabu ya Azam FC, Prince Dube, ameingia kwenye vitabu vya historia ya timu hiyo akifanikiwa kuwa mfungaji bora namba nane.

Dube ameingia kwenye historia hiyo baada ya kuibuka mfungaji bora wa Azam FC msimu ulioisha 2020/2021 akifunga jumla ya mabao 14, akizidiwa mawili tu na mfungaji bora wa ligi, John Bocco ‘Adebayor’, aliyetupia 16.

Nyota huyo kutoka Zimbabwe, aliyesajiliwa msimu huu akitokea Highlanders ya huko, ameandika rekodi nyingine ya kuwa mshambuliaji pekee aliyehusika kwenye mabao mengi kwenye mashindano ya ndani msimu ulioisha, akiwa amehusika katika mabao 22, akifunga 17 (14 VPL, 3 FA Cup) huku akitoa pasi za mwisho tano.

Wafungaji saba waliopita Azam FC  

Msimu wa kwanza Azam FC ilipocheza kwa mara ya kwanza Ligi Kuu 2008/2009, mfungaji wetu bora wa klabu alikuwa ni Nsa Job, aliyefunga mabao tisa, huku msimu wa 2009/2010 akiwa Bocco baada ya kufunga mabao 14.

Takwimu za mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Kipre Tchetche, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2012/2013.

Mrisho Ngassa, aliyejiunga nasi kwa rekodi ya usajili akitokea Yanga, aliibuka kinara wa mabao kwenye klabu yetu na mfungaji bora wa ligi msimu wa 2010/2011 akifunga 16, kabla ya Bocco aliyetupia 19 na Kipre Tchetche 17, kufuatia misimu iliyofuata (2011/2012, 2012/2013), ambao nao waliibuka wafungaji bora kwenye ligi pia.

Tchetche akawa mfungaji bora tena kwenye timu hii wakati tunabeba ubingwa wa ligi 2013/2014 akifunga 13, huku Didier Kavumbagu, akiwa mfungaji wetu bora msimu 2014/2015 kwa mabao yake 10.

Takwimu za kiungo mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, Mrisho Ngassa, alipoibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2010/2011.

Wafungaji wengine;

2015/16 | Kipre Tchetche | 12 ⚽

2016/17 | John Bocco | 9 ⚽

2017/18 | Shaaban Chilunda | 10 ⚽

2018/19 | Donald Ngoma | 11 ⚽

2019/20 | Obrey Chirwa | 12 ⚽