KIUNGO mshambuliaji wa Klabu ya Azam, Idd Seleman ‘Nado’, ameandika rekodi ya kuwa mchezaji pekee mzawa aliyehusika kwenye mabao mengi kwenye ligi msimu ulioisha 2020/2021.

Nado amewafunika kabisa wachezaji wenzake wa Kitanzania, baada ya kuhusika kwenye mabao 19, akiwa amefunga 10 na kutoa pasi za mwisho tisa, akimzidi mfungaji bora wa ligi, John Bocco ‘Adebayor’, aliyesaidia mabao 18 katika kikosi cha Simba, akitupia nyavuni mara 16 na pasi za mwisho mbili.

Nyota huyo tuliyemsajili kutoka Mbeya City misimu miwili iliyopita, amekuwa kwenye kiwango bora akiwa ndiye mfungaji bora namba mbili wa timu yetu msimu uliopita kwa mabao yake 10, nyuma ya mfungaji wetu bora, Prince Dube, aliyetupia 14 katika ligi.

Kiungo mshambuliaji, Idd Seleman ‘Nado’, akifunga moja ya mabao yake msimu uliopita dhidi ya Namungo kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Aidha, Nado ameshika namba moja kwa kutoa pasi za mwisho kwenye timu yetu, akifanya hivyo mara tisa huku Dube akiwa namba mbili kwa pasi zake tano alizochangia.