KLABU ya Azam imepangwa Kundi B sambamba na timu za Tusker (Kenya) na Atlabara (Sudan Kusini) kwenye fainali za michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup).
Michuano hiyo inatarajia kuanza kutimua vumbi kuanzia Agosti Mosi hadi 15 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.
Azam FC tutashiriki michuano hii yenye historia kubwa barani Afrika, tukiwa tumeingia fainali tatu mfululizo zilizopita na kutwaa taji hili mara mbili mfululizo (2015, 2018).
Mwaka 2015, tulipotwaa mara ya kwanza tuliifunga Gor Mahia ya Kenya mabao 2-0, yaliyofungwa na nyota wetu wa zamani, nahodha John Bocco na Kipre Tchetche, mchezo uliofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Tukarudia historia yetu nzuri ya kutwaa taji bila kupoteza mchezo kwa kucheza fainali ya pili mfululizo na kutetea taji letu mwaka 2018, tukikipiga dhidi ya Simba na kuichapa mabao 2-1, yaliyowekwa kimiani na Nahodha Agrey Moris kwa mkwaju wa adhabu ndogo ya moja kwa moja, kabla ya Shabaan Chilunda kutupia msumari wa pili.

Mwaka juzi tuliingia fainali ya tatu mfululizo kwenye michuano iliyofanyika jijini Kigali, Rwanda kikosi cha Azam FC kikiundwa na wachezaji wengi vijana na kupoteza kwenye fainali kwa kufungwa na mabingwa wa sasa KCCA ya Uganda bao 1-0.
Aidha Azam FC, kabla ya kutinga fainali iliichapa miamba ya Afrika, TP Mazembe mabao 2-1 kwenye mchezo wa robo fainali na nusu fainali ikaiondoa Maniema kwa mikwaju ya penalti 5-4.