KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imejiongezea pointi moja kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) baada ya kutoka suluhu dhidi ya KMC mchezo uliomalizika usiku huu katika Uwanja wa Azam Complex.

Pointi hiyo inaifanya Azam FC kufikisha pointi 68 kwenye msimamo wa ligi ikiwa nafasi ya tatu, ikizidiwa pointi 13 na vinara Simba waliojikusanyia 81 huku Yanga walio nafasi ya pili wakiwa nazo 80.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake, Azam FC ikionekana kutengeneza nafasi nyingi zaidi za kufunga mabao lakini ikishindwa kuzitumia katika kipindi cha kwanza na pili.

Mshambuliaji kinda anayekuja vizuri, Paul Peter, aliyeanza kwenye mchezo huo, alipata nafasi nzuri dakika ya 20 ya kuipa bao la uongozi Azam FC, kufuatia uzembe wa safu ya ulinzi ya KMC, lakini shuti alilopiga akiwa anatazamana lango lilitoka sentimita chache.

Kipindi cha pili winga Enock Atta, aliyekuwa kwenye kiwango kizuri, alikosa nafasi mbili za wazi moja akipiga shuti lililomlenga kipa na nyingine akipiga shuti lililopaa juu ya lango, kabla ya kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, naye kukosa dakika za mwisho akipokea krosi ya Danny Lyanga na kupiga shuti lililookolewa kwenye mstari na mabeki wa KMC.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kushuka tena dimbani Jumatatu ijayo kukabiliana na Simba katika muendelezo wa ligi hiyo, utakaopigwa Uwanja wa Uhuru saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC:

Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Daniel Amoah, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya/Stephan Kingue dk 64, Enock Atta/Idd Kipagwile dk 85, Frank Domayo, Paul Peter/Tafadzwa Kutinyu dk 51, Danny Lyanga, Salum Abubakar