BEKI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Yakubu Mohammed, amesaini mkataba mpya wa miaka miwili leo alhamisi.

Awali mkataba wa Yakubu ulikuwa ukitarajia kumalizika Novemba mwaka huu, hivyo kwa kuongeza mkataba huo kutamfanya aendelea kuitumikia Azam FC hadi 2021.

Nyota huyo amekuwa na kiwango kizuri tokea ajiunge na Azam FC Novemba 2016, akitokea Aduana Stars ya Ghana, ambapo kwa mara ya kwanza alisaini mkataba wa miaka mitatu.

Beki huyo raia wa Ghana, amesaini mkataba huo mbele ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Abdulkarim Amin, Mratibu wa timu, Phillip Alando na Wakala wake, Joseph Epton.

Mara baada ya kusaini mkataba huo, Yakubu amesema kuwa anajisikia furaha kusaini mkataba mpya akidai Azam FC ni kama familia.

“Kwa mashabiki, kila siku tunafanya kazi kwa bidii ili kuwafurahisha na naamini huu mwaka tutawapa furaha kubwa usoni kwao kwa kufuzu kwa Kombe la Shirikisho Afrika kwa kushinda Kombe la FA, hivyo Inshallah tunawaahidi hili kombe, wote wanatakiwa kuja kwenye fainali kwenda kushuhudia na kutupa sapoti,” alisema huku akiwa na uso wa furaha.

Huo ni mwendelezo wa uongozi wa Azam FC kurefusha mikataba ya wachezaji inayofikia ukingoni ili kutengeneza kikosi bora cha ushindani msimu ujao, hadi sasa ukiondoa Yakubu walioongeza mikataba ni mshambuliaji Donald Ngoma, mabeki Bruce Kangwa, Abdallah Kheri, David Mwantika na winga Joseph Mahundi.