BAADA ya kutoka sare kwenye mchezo wa juzi dhidi ya Stand United ugenini, kikosi cha Azam FC kitashuka dimbani tena kuvaana na KMC katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaopigwa Uwanja wa Azam Complex kesho Alhamisi saa 1.00 usiku.

Azam FC itacheza mchezo huo ikiwa ni baada ya siku moja tu tokea irejee kutoka mkoani Shinyanga jana ilipotoka sare ya bao 1-1, bao la matajiri hao likiwekwa kimiani na mshambuliaji Danny Lyanga kwa shuti kali akiunganisha pasi ya juu ya kiungo Mudathir Yahya.

Mabingwa hao wataingia dimbani wakiwa na kikosi chao chote, baada ya kurejea kwa nyota wake nahodha Agrey Moris, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, Bruce Kangwa na Yakubu Mohammed, ambao walikosa mchezo uliopita baada ya kukusanya kadi tatu za njano.

Benchi la ufundi la timu hiyo limejipanga vilivyo kumaliza vema mechi nne zilizobakia kwenye ligi kabla ya kuelekea kwenye mechi ya mwisho ya msimu ya fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) itakayocheza dhidi ya Lipuli kwenye Uwanja wa Ilulu, mkoani Lindi.

Itakumbukwa kuwa hii ni mara ya pili kwa Azam FC kukutana na KMC kwenye ligi, katika raundi ya kwanza zilitoka sare ya mabao 2-2, mabao ya matajiri hao yakiwekwa kimiani na kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu na mshambuliaji Donald Ngoma.

Lakini itakuwa ni mara ya tatu kukutana kwenye mashindano yote msimu huu, mchezo mwingine ukiwa ni nusu fainali ya Kombe la FA, Azam FC ilipotinga fainali kwa kuichapa KMC bao 1-0, lililowekwa kimiani na Ngoma wiki iliyopita, akiunganisha pande safi la beki wa kulia Nickolas Wadada.

Hadi sasa ligi ikiwa inaelekea ukingoni, Azam FC imefanikiwa kucheza mechi 34 ikiwa imejikusanyia pointi 67 katika nafasi ya tatu kwenye msimamo, ikizidiwa pointi 14 na Simba iliyokileleni ikiwa nazo 81, Yanga nafasi ya pili ikijizolea 80.