KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imevuna pointi moja jioni ya leo Jumatatu baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Stand United, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kujiongezea pointi moja, ikifikisha 67 kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa nafasi ya tatu, ikizidiwa pointi 13 na vinara Yanga waliofikisha 80 huku Simba iliyocheza mechi 30 ikiwa nafasi ya pili ikijizolea 78.

Azam FC ilianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao la uongozi dakika 17 lililofungwa kwa shuti zuri la pembeni na mshambuliaji Danny Lyanga, akiunganisha pasi ndefu ya juu ya kiungo Mudathir Yahya.

Lyanga alijaribu tena kuipatia bao la pili Azam FC, dakika ya 31 baada ya kupiga kichwa kizuri kilichogonga mwamba wa juu na mpira kurudi ndani kabla ya mabeki wa Stand United kuokoa na hivyo hadi kipindi cha kwanza kinamalizika, matajiri hao waliondoka kifua mbele kwa bao hilo.

Dakika ya 70, kiungo Hafidh Mussa, aliisawazishia Stand United kwa shuti zuri nje ya eneo la 18 na kufanya dakika 90 kumalizika kwa sare hiyo, Azam FC ikiwa imefanikiwa kukusanya pointi nne dhidi ya Stand kutokana na ushindi wa 3-1 kwenye mchezo wa raundi ya kwanza uliofanyika Azam Complex.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea Dar es Salaam kesho Jumanne, tayari kuanza maandalizi ya mchezo ujao wa ligi dhidi ya KMC utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Mei 9 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC leo:

Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Hassan Mwasapili, Daniel Amoah, Lusajo Mwaikenda, Stephan Kingue, Enock Atta/Joseph Kimwaga dk 85, Mudathir Yahya (C), Danny Lyanga, Obrey Chirwa/Paul Peter dk 61, Ramadhan Singano/Idd Kipagwile dk 57