KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimeshawasili salama mjini Shinyanga usiku wa jana, tayari kwa kazi moja tu ya kupambana na Stand United kwenye mwendelezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) kesho Jumatatu saa 10.00 jioni.

Mchezo huo unatarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na ushindani wa timu hizo kila zinapokutana ndani ya Uwanja Kambarage, Azam FC ikijipanga kufanya kweli ili kuendelea kujiweka sawa katika msimamo wa ligi hiyo.

Wachezaji wa Azam FC wote wapo kwenye hali nzuri, lakini benchi la ufundi la timu hiyo limejipanga kufanya mabadiliko kadhaa kuelekea mchezo huo ili kukabiliana na tatizo la baadhi ya wachezaji kukusanya kadi tatu za njano, hivyo moja kwa moja kutoruhusiwa kucheza mechi hiyo.

Kikosi cha Azam FC kitashuka dimbani kikiwa na kumbukumbu ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya juzi kuichapa KMC bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Donald Ngoma, ambaye yupo fiti kabisa tayari kwa kipute hicho kingine muhimu.

Timu hizo kihistoria zimekutana mara saba kwenye mechi za ligi tokea Stand United ipande daraja mwaka 2015, Azam FC imeshinda mara tano na kupoteza mara mbili huku kukiwa hamna sare yoyote iliyowahi kupatikana.

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, wanahistoria ya kushinda mechi moja tu kwenye Uwanja wa Kambarage dhidi ya Stand United ikishinda 2-0 msimu wa 2015/2016, yaliyofungwa na Allan Wanga na Frank Domayo, lakini baada ya hapo imepoteza mechi mbili mfululizo katika uwanja huo.

Mara ya mwisho kukutana kwenye Uwanja wa Azam Complex msimu huu, Azam FC ilishinda mabao 3-1, yaliyofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wake, Yahya Zayd, aliyetupia mawili huku winga Enock Atta, akitupia jingine.