KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imekuwa timu ya kwanza kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) msimu huu baada ya kuichapa KMC bao 1-0 usiku huu.

Fainali ya michuano hiyo msimu huu inatarajia kupigwa kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi, Juni 2 mwaka huu, ambapo Azam FC inasubiri kukutana na mshindi wa mechi nyingine ya nusu fainali kati ya Yanga na Lipuli inayotarajia kufanyika keshokutwa Jumapili.

Hii ni mara ya pili kwa Azam FC kutinga kwa fainali hiyo, mara ya kwanza ilikuwa msimu wa 2015/2016, ilipocheza na Yanga na kufungwa mabao 3-1, bao la matajiri hao likiwekwa kimiani na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Didier Kavumbagu.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake, ambapo Azam FC ilianza kwa kasi na kutengeneza nafasi mbili nzuri dakika 18 za mwanzo, lakini kipa wa KMC, Jonathan Nahimana, aliweza kupangua michomo ya Obrey Chirwa na Yakubu Mohammed,

Bao pekee la Azam FC liliwekwa kimiani na mshambuliaji Donald Ngoma, dakika ya 73, akimalizia krosi safi ya chini ya beki wa kulia, Nickolas Wadada.

Hilo ni bao la 13 kwa Ngoma msimu huu kwenye michuano yote, akiwa ndio mfungaji bora wa Azam FC msimu huu hadi sasa.

Hata hivyo, mshambuliaji huyo raia wa Zimbabwe, hawakuweza kumaliza mchezo huo baada ya kuumia na nafasi yake ilichukuliwa na Danny Lyanga, dakika ya 85.

Azam FC imejiwekea malengo ya kutwaa ubingwa huo msimu huu ili kurejea kwenye michuano ya Afrika msimu ujao baada ya kuikosa kwa miaka miwili, ambapo ikiweza kutwaa taji hilo itashiriki Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup).

Kikosi cha Azam FC:  

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Joseph Mahundi, Frank Domayo, Obrey Chirwa, Salum Abubakar/Mudathir Yahya dk 90, Ramadhan Singano/Donald Ngoma dk 55/Danny Lyanga dk 85