SAFARI ya Azam FC, kutinga fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) inatarajia kuhitimika kwa mchezo wa nusu fainali dhidi ya KMC utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Ijumaa saa 1.00 usiku.

Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, wamekuwa na mwenendo mzuri kwenye michuano hiyo msimu huu kama ilivyo kwa wapinzani wao KMC, ambapo inatarajia kuwa mechi ya ushindani mkubwa kwa pande zote mbili.

Azam FC ilitinga hatua hiyo baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0 lililofungwa na Joseph Mahundi, akiunganisha pande la Stephan Kingue, huku KMC nayo ikiichapa African Lyon 2-0 na kutinga hatua hiyo.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye hali nzuri kabisa kuelekea mechi hiyo, picha ya kutofanya vema kwenye michezo miwili iliyopita ya ligi, ambapo wachezaji wamepanga kupambana kuhakikisha wanashinda na kutinga fainali ya michuano hiyo.

Nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, aliyekosa mechi tatu zilizopita akitumikia adhabu ya kadi nyekundu atakuwa akirejea dimbani baada ya kumaliza adhabu hiyo, akitarajia kuongeza nguvu zaidi kwenye eneo la ulinzi.

Aidha ikifanikiwa kutinga fainali ya michuano hiyo, itakuwa ni kwa mara ya pili kufanya hivyo, mara ya kwanza ikiwa msimu wa 2015/2016 ilipotinga na kukutana na Yanga, kabla ya kufungwa mabao 3-1, bao pekee la Azam FC likiwekwa kimiani na mshambuliaji wa zamani, Didier Kavumbagu.

Licha ya Azam FC kukutana na KMC kwenye ligi na kutoka sare ya mabao 2-2, timu hizo zimewahi kukutana kwenye hatua ya 16 bora ya michuano hiyo msimu uliopita, na Azam FC kuibuka kidedea kwa ushindi wa 3-1, huku ikishuhudiwa Nahodha Msaidizi, Frank Domayo, Mbaraka Yusuph na Yahya Zayd.

Wababe hao wa Chamazi, wamejipanga vilivyo kuhakikisha wanaingia fainali na kutwaa ubingwa huo ili kuhakikisha wanarudi kwenye michuano ya Afrika msimu ujao, kwani bingwa wa ASFC ataiwakilisha nchi katika Kombe la Shirikisho Afrika.

Fainali ya michuano hiyo mwaka huu, inatarajia kufanyika kwenye Uwanja wa Ilulu mkoani Lindi Juni 2 mwaka huu, bingwa akitarajia kuvuna kikombe, medali za dhahabu na Sh. milioni 50.  

Nusu fainali nyingine ya michuano hiyo itawahusisha, Lipuli watakaoikaribisha Yanga, mchezo utakaopigwa Mei 5 mwaka huu kwenye Uwanja wa Samora, Iringa.