KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeshindwa kufanya kweli baada ya kupigwa bao 1-0 dhidi ya Yanga, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Uhuru.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kubakia nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa na pointi 66, ikizidiwa pointi 11 na kinara Yanga aliyefikisha 77.

Mchezo huo ulikuwa mkali na wa aina yake, Yanga ikionekana kushambulia kupitia mashambulizi ya kushtukiza, na kutangulia kwa bao dakika ya 13 lililofungwa na winga Mrisho Ngassa, aliyetumia krosi ya chini ya Ibrahim Ajibu.

Azam FC iliyofanikiwa kutawala mchezo ilijitahidi kuswazisha bao hilo, kupitia kwa wshambuliaji wake Obrey Chirwa na Donald Ngoma, lakini mashuti yao yalishindwa kutinga nyavuni na kuishia kutoka nje ya lango.

Mshambuliaji Danny Lyanga, aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Ngoma, alikosa nafasi ya wazi akiwa anatazamana na kipa wa Yanga, Clouds Kindoki, lakini mpira wa kunyanyua alioupiga ulienda nje ya lango.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kesho Jumanne kinatarajia kuanza maandalizi kuelekea mtanange ujao wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya KMC utakaofanyika Machi 3 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.

Kikosi cha Azam FC leo;

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda, Yakubu Mohamed, Stephan Kingue, Joseph Mahundi/Ennock Atta dk76, Mudathir Yahya, Donald Ngoma/Danny Lyanga dk 72, Obrey Chirwa, Salum Abubakar ‘Sure Boy’.