UONGOZI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, unapenda kukanusha vikali taarifa zinazoendelea kusambaa kwenye mitandao ya kijamii kuwa kiungo Salum Abubakar ‘Sure Boy’, amepokea fedha kutoka kwa kiongozi mmoja wa Yanga.

Taarifa hiyo ye kutengenezwa inasambaa wakati ikiwa imebakia siku moja kabla ya Azam FC haijacheza na Yanga kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) unaotarajia kufanyika Uwanja wa Uhuru, kesho Jumatatu kuanzia saa 10.00 jioni.

Ujumbe huo unaeleza kuwa “Mchezaji wa Azam atumiwa milioni 3 na mjumbe wa Yanga.

Mchezaji wa Azam, Sure Boy, amekutwa na milioni 3 kutoka kwenye namba ya mmoja kati ya wajumbe wa kamati iliyoteuliwa ya muda ya Yanga, mjumbe huyo ambaye jina tunalo (tutalitoa mkihitaji) alituma pesa hizo juzi majira ya saa 3:52:23 kupitia kwa wakala mwenye jina la Thobias Kiwavi jijini Dar.

Ikumbukwe kuwa Yanga wana mechi na Azam siku ya Jumatatu,” ilinukuliwa kutoka chanzo cha Sports EM.

Azam FC tunaamini ya kuwa taarifa hizi ni uzushi mtupu na zinakuja ili kumwondoa mchezoni mchezaji wetu na kuwachanganya wachezaji wetu kuelekea mechi hiyo, hivyo tunawaomba mashabiki wetu mzipuuze.

“Uongozi wa Azam FC unaoenda kuutahadharisha umma kuwa uzushi unaoendelea kwa mchezaji wetu, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, kuwa amepokea pesa Tsh 3,000,000 kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Yanga unafaa kupuuzwa na kwamba una nia mbaya kwa mchezaji wetu,” uongozi wa Azam FC ukitolea ufafanuzi suala hilo.