KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itakuwa kibaruani kuvaana na Yanga, kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) unaotarajia kufanyika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kesho Jumatatu saa 10.00 jioni.

Mtanange huo unatarajiwa kuwa mkali na wa aina yake kutokana upinzani wa timu hizo kila zinapokutana, wachezaji wa Azam FC wakiwa na morali ya hali ya juu tayari kuvuna pointi tatu muhimu.

Licha ya ligi kufikia mechi za lala salama kwenye mzunguko wa pili, lakini huo utakuwa ni mchezo wa kwanza msimu huu kwa timu hizo kikiwa ni kiporo cha mzunguko wa kwanza.

Timu zote zitaingia dimbani zikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi zao zilizopita, Azam FC ikiteleza kwa kufungwa na Ndanda (1-0) ugenini huku Yanga nayo ikifungwa na Mtibwa Sugar (1-0).

Azam FC itazidi kujiimarisha kwenye mchezo huo, pale itakapowapokea wachezaji wake watatu waliokuwa wamefungiwa mechi tatu, viungo Stephan Kingue, Tafadzwa Kutinyu na winga Ramadhan Singano, lakini itaendelea kumkosa nahodha wake, Agrey Moris, atakayekuwa akitumikia mechi yake ya mwisho katika adhabu ya kukosa mechi tatu kufuatia kadi nyekundu aliyoipata dhidi ya Mbao.

Benchi la ufundi la Azam FC chini ya makocha wazawa, Meja Mstaafu Abdul Mingange na Idd Nassor Cheche, limeahidi kufanya kweli kwenye mchezo huo, likiwa na malengo makuu ya kumaliza ligi ikiwa nafasi mbili za juu kwenye msimamo.

Takwimu zinaonyesha kuwa, huo utakuwa ni mchezo wa 21 kwa timu hizo kukutana kwenye ligi, ambapo kwenye mechi 20 zilizopita, wababe hao kutoka viunga vya Azam Complex, wamefanikiwa kushinda mara sita, Yanga ikishinda saba na saba nyingine zikienda sare.

Makocha hao hao waliokuwemo kwenye benchi la ufundi la Azam FC hivi sasa, ndio waliiongoza timu hiyo kumaliza nafasi ya pili msimu uliopita, ambayo ilipatikana baada ya kuiongoza kuichapa Yanga mabao 3-1 katika mchezo wa mwisho wa ligi, yaliyofungwa na Yahya Zayd, Shaaban Idd na Salum Abubakar ‘Sure Boy’.