KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, ilipata ugeni mkubwa jioni ya leo Ijumaa, baada ya kutembelewa na mawakala mbalimbali akiwemo Sebastian Arnesen wa Manchester City walioweza kumulika wachezaji wa timu hiyo.

Ugeni huo uliongozwa na mmoja wa Wakurugenzi wa Azam FC, Yusuf Bakhresa, ambaye ndiye aliyewaleta kwenye viunga vya Azam Complex, kwa ajili ya manufaa ya baadaye ya wachezaji wa timu hiyo kutafutiwa masoko barani Ulaya.

Arnesen na jopo lake, waliweza kushuhudia mechi maalum iliyoandaliwa baina ya timu kubwa ya Azam FC na ile ya vijana chini ya umri wa miaka 20 (Azam U-20) iliyoisha kwa sare ya mabao 2-2, ambapo waliweza kuridhishwa na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo ya vijana.

Familia ya Bakhresa ambayo ndiyo wamiliki wa timu hiyo, wamekuwa wakijitahidi kuwekeza vema kwenye soka la vijana kupitia kituo cha kukuza vipaji walichokianzisha, lengo kubwa ni kutoa ajira kwa vijana na kusaidia maendeleo ya soka nchini.

Katika jitihada hizo walizozianzisha, mwanga umeanza kuonekana hadi sasa wachezaji waliowahi kupita kwenye kituo hicho wamekuwa wakitamba kwenye timu mbalimbali nchini na wengine wakishiriki kwenye harakati za kusaidia timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika mwaka huu nchini Misri.

Wachezaji ambao hadi sasa Azam FC imefanikiwa kuwauza nje ya nchi kupitia kituo chake ni aliyekuwa nahodha wa timu hiyo, Himid Mao ‘Ninja’, ambaye sasa anakipiga kwa mafanikio nchini MIsri katika timu ya Petrojet, mshambuliaji Yahya Zayd alinunuliwa na miamba Ismaily kutoka nchini humo na wengine wawili wakiwa barani Ulaya, winga Farid Mussa, anayekipiga CD Tenerife ya Hispania na mshambuliaji Shaaban Idd, aliyekuwa kwa mkopo CD Izarra akitokea Tenerife.