KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeanza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Yanga, huku Uwanja wa mechi hiyo ukibadilishwa kutoka ule wa Taifa na sasa ukitarajia kupigwa ule wa Uhuru Jumatatu hii saa 10.00 jioni.

Kwa mujibu wa barua iliyotumwa na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB) imeeleza kuwa mabadiliko hayo ya uwanja yanatokana na uwanja huo kutarajiwa kufungwa mara baada ya kumalizika kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17, yakitarajia kumalizika Jumapili hii nchini.

Azam FC imeanza mazoezi ikiwa na kikosi kamili, ambapo kwa mujibu wa programu kikosi hicho kinatarajia kujifua kwa siku sita hadi kuelekea mtanange huo, ambao utakuwa ni wa kwanza kwa timu zote kukutana kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) msimu huu.

Kikosi hicho ndani ya siku hizo sita za mazoezi, kitajifua mara moja kila siku jioni, isipokuwa keshokutwa Alhamisi kikitarajia kufanya mara mbili asubuhi na jioni huku Ijumaa hii kikitarajia kucheza mchezo wa kujiweka sawa dhidi ya timu ya vijana ya Azam FC.