KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeteleza kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona baada ya kupoteza kwa kufungwa na Ndanda bao 1-0, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika jioni ya leo.

Huo unakuwa mchezo wa tatu kwa Azam FC kupoteza msimu huu, na mechi ya kwanza kupoteza baada ya mechi nane mfulululizo kupita za mashindano, mechi nyingine ilizopoteza ni dhidi ya Mtibwa Sugar na Simba, zote ikicheza nje ya viunga vya Azam Complex.

Matokeo yanaifanya Azam FC kubakiwa na pointi zake 66 kwenye msimamo wa ligi, ikiwa nafasi ya pili ikizidiwa point inane Yanga iliyonazo 74 huku Simba iliyocheza mechi 23 katika nafasi ya tatu ikijizolea 60.

Azam FC ilipata nafasi nzuri dakika ya 19 baada ya kona iliyochongwa na Mahundi, kumkuta beki Yakubu Mohammed, aliyepiga kichwa kilichotoka pembeni kidogo ya lango.

Bao pekee la Ndanda limefungwa dakika ya 62 na Mohamed Mkopi, ambalo lilidumu hadi mwisho wa mchezo huo uliochezeshwa na mwamuzi Shakaile Ole Yanga Lai.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kuanza safari ya kurejea jijini Dar es Salaam, kesho alfajiri tayari kwa maandalizi ya mchezo ujao wa ligi itakaocheza dhidi ya Yanga Aprili 29 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda, Yakubu Mohammed, Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Enock Atta dk 56, Frank Domayo (C), Donald Ngoma, Danny Lyanga/Hamis Ngoengo dk 71, Salum Abubakar