BAADA ya kutoka kuichapa Mbeya City, Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, itashuka tena dimbani kuvaana na Ndanda, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaofanyika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara kesho Alhamisi saa 10.00 jioni.

Tayari kikosi cha Azam FC kimeshawasili mkoani humo tokea jana, wachezaji wote wakiwa kwenye hali nzuri kabisa, ambapo jioni ya leo Jumatano kitafanya mazoezi ya mwisho kwenye dimba hilo.

Azam FC ambayo tayari imeshacheza mechi 31 za ligi, imetoka kuichapa Mbeya City bao 1-0 ugenini kwenye mchezo uliopita, huku Ndanda ikipata ushindi kama huo nyumbani dhidi ya Coastal Union.

Mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na Kagame (CECAFA Kagame Cup) msimu huu, itanufaika na urejeo wa mshambuliaji Donald Ngoma, aliyeukosa mchezo uliopita kutokana na kutumikia na adhabu ya kukusanya kadi tatu za njano.

Benchi la ufundi la timu hiyo limejipanga vema likiwa na mwendelezo wa matokeo bora, wakishinda mechi saba kati ya nane zilizopita, mchezo mwingine ukiwa ni suluhu iliocheza ugenini dhidi ya Mbao, ikiwa imefunga jumla ya mabao 20 na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara mbili tu.  

Kihistoria Azam FC iliyopanda rasmi Ligi Kuu mwaka 2008, imekutana na Ndanda mara tisa kwenye mechi za ligi, ikishinda mara sita, sare moja na kupoteza mbili, zote zikiwa ugenini.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana mjini Mtwara, Azam FC ilishinda bao 1-0, lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji wa timu, Yahaya Mohammed, aliyekuwa akiunganisha krosi ya beki wa kushoto Bruce Kangwa.

Aidha zilipokutana kwenye raundi ya kwanza msimu huu, Azam FC ilishinda mabao 3-0, yaliyofungwa na kiungo Tafadzwa Kutinyu, aliyetupia mawili huku winga Joseph Mahundi akitupia jingine la mwisho.