KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imefanya kweli mkoani Mbeya baada ya kuichapa Mbeya City bao 1-0, mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Sokoine, Mbeya leo jumapili.

Ushindi huo unaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 66 kwenye msimamo wa ligi ikiwa nafasi ya pili ikizidiwa pointi nane na kinara Yanga aliyekuwa nazo 74, Simba iliyocheza mechi 22 ni ya tatu ikijikusanyia 57.

Mabingwa hao wa Kombe la Kagame na Kombe la Mapinduzi msimu huu, waliingia kwenye mchezo huo wakiwakosa nyota wake kadhaa, nahodha Agrey Moris, anayetumikia adhabu ya kadi nyekundu, mshambuliaji Donald Ngoma, mwenye kadi tatu za njano, mshambuliaji Obrey Chirwa, aliyepata msiba nchini kwao Zambia na beki David Mwantika, aliyekuwa majeruhi.

Wachezaji wengine waliokuwa wakitumikia adhabu ni kiungo mshambuliaji, Tafadzwa Kutinyu, Stephan Kingue na winga Ramadhan Singano, ambao walifungiwa mechi tatu kuanzia mechi iliyopita dhidi ya Mbao, wakidaiwa kumzonga mwamuzi Athuman Lazi, wakati Azam FC ikimenyana na Coastal Union jijini Tanga.

Azam FC ilionekana kucheza vizuri muda wote wa mchezo licha ya kuwa pungufu ya mchezaji mmoja dakika 30 za mwisho za mchezo huo baada ya mshambuliaji Paul Peter, kuonyeshwa kadi nyekundu yenye utata na mwamuzi Florentina Zablon kutoka Dodoma dakika ya 60.

Beki wa Azam FC, Yakubu Mohammed, aliyeonekana kucheza vema kwenye eneo la beki ya kati sambamba na beki chipukizi kutoka Azam Academy, Lusajo Mwaikenda, ndiye aliyeipatia bao pekee timu hiyo dakika ya 45 akimalizia krosi iliyopigwa na kiungo, Mudathir Yahya, kufuatia mpira wa kona alioanzishiwa na Bruce Kangwa.

Azam FC kwa kushinda mechi hiyo, inakuwa imevuna pointi zote sita dhidi ya Mbeya City msimu huu, baada ya raundi ya kwanza kuinyuka mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Azam Complex, mabao yaliyofungwa na mshambuliaji Danny Lyanga na Joseph Mahundi.

Mara baada ya ushindi huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho Jumatatu mchana kwa usafiri wa ndege, na Jumanne kitaanza safari nyingine kuelekea mkoani Mtwara kukipiga na Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Aprili 18 mwaka huu

Kikosi cha Azam FC:

Razak Abalora, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda, Yakubu Mohammed, Mudathir Yahya, Joseph Mahundi/Idd Kipagwile dk 89, Frank Domayo/Salmin Hoza dk 80, Paul Peter (red card dk 60), Danny Lyanga, Salum Abubakar