KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimetua salama jijini Mbeya leo Jumamosi tayari kukabiliana na Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) unaotarajia kufanyika Uwanja wa Sokoine, Mbeya kesho Jumapili saa 10.00 jioni.

Wachezaji wamewasili wakiwa na morali ya hali ya juu tayari kufanya kweli kuhakikisha wanvuna pointi zote tatu kwenye mchezo huo, unaotarajia kuwa mkali na wa aina yake.

Matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex, wameambatana na wachezaji watatu kutoka timu ya vijana ya timu hiyo, beki wa kulia, Samwel Onditi, kiungo Omary Banda na mshambuliaji Hamis Ngoengo, ambao wanaongeza nguvu kuziba mapengo ya baadhi ya wachezaji watakaokosekana.

Wakati Azam FC ikitoka kutoka suluhu kwenye mchezo uliopita dhidi ya Mbao uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, wapinzani wao Mbeya City waliokuwa wakicheza nyumbani katika dimba la Sokoine waliichapa KMC bao 1-0.

Kocha wa timu hiyo, Meja Mstaafu Abdul Mingange, amesema kuwa vijana wanaari kubwa ya kusaka ushindi huku akidokeza kuwa wamejipanga kufanya vizuri.

“Matarajio yetu sisi ni kushinda tu hatuna njia nyingine tumejitayarisha vizuri na timu yetu ni timu kubwa na tunaposafiri tunapambana ili tulete heshima kwenye timu yetu,” alisema.

Kihistoria Azam FC na Mbeya City zimekutana mara 11 kwenye ligi, tokea timu hiyo ya jijini Mbeya ilivyopanda daraja mwaka 2013, Azam FC ikiwa imeshinda asilimia 95 ya mechi zote ikiibuka kidedea mara sita, sare nne na kupoteza mara moja.

Mchezo ilioupoteza ilitokana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuipoka pointi tatu Azam FC baada ya kushinda mabao 3-0 jijini Mbeya, ikidai ilimchezesha beki Erasto Nyoni kimakosa kutokana na mchezaji huyo kukusanya kadi tatu za njano.  

Mara ya mwisho timu hizo kukutana kwenye raundi ya kwanza, Azam FC ilishinda mabao 2-0, yaliyowekwa kimiani na winga Joseph Mahundi na mshambuliaji, Danny Lyanga.