KOCHA wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Idd Nassor Cheche, amekiri ushindani ni mkubwa kwenye kikosi hicho hali inayochangia matokeo bora uwanjani.

Kikosi cha Azam FC kimekuwa kwenye mwenendo mzuri hivi sasa, kikishinda mechi sita mfululizo na kutoka sare moja tokea ichukuliwe na benchi jipya la ufundi chini ya Meja Mstaafu, Abdul Mingange na Cheche.

Akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz, Cheche aliwapongeza wachezaji wake kutokana na hali hiyo akidai kuwa ni jambo ya furaha kuona wanatambua wajibu wao katika kuipigania timu hiyo.

“Kwanza nafurahi kwa kuwa wachezaji wote wana ari na kila mtu anaonesha ushindani na kila mtu analilia nafasi ya kuanza yeye, sasa hili ni jambo ambalo linatupa moyo sisi benchi la ufundi kwamba kuona kila mtu anapambana kuipambania nafasi, kwa hiyo ukimuona mtu anapambania nafasi na kuipigania timu yake itakuwa ni rahisi kabisa,” alisema.

Akizungumzia muendelezo wa kuwapa wachezaji wote nafasi kwenye mechi zinazoendelea, alisema kuwa; “Unapokuwa na kundi la watu zaidi ya 11, tuseme timu inayoanza ndani ni watu 11, lakini usajili unafika watu 25 mpaka 30, sasa unapotumia wachezaji wachache katika mechi kila siku ndio hao hao na kushindwa kufanya ‘rotation’, basi unawaua watu wengine wale ambao hawapati nafasi na wale wanaopata nafasi vile vile unawaua.

“Kwa sababu ili wale wapate nafasi ina maana lazima wafanye mazoezi na wenzao, hasa wenzao wakiwa wapo chini basi wao hawawezi kuonesha kutoa mafanikio kwa sababu anafanya mazoezi na mtu ambaye yupo chini, lakini kukiwa na ushindani kila mtu anashindania nafasi na kila mtu anaona mimi nikifanya hili nitapata nafasi, basi unapata timu yenye ushindani na vile vile unapata matokeo katika michezo yako,” alisema.

Kikosi cha Azam FC tayari kimeanza rasmi mazoezi tokea juzi kikijiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Mbeya City utakaofanyika keshokutwa Jumapili kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.

Katika kujiandaa vema na mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitafanya mazoezi ya mwisho jijini Dar es Salaam leo Ijumaa jioni kabla ya kesho Jumamosi asubuhi kuanza safari ya kuelekea jijini Mbeya kwa usafiri wa ndege.