KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, leo Jumatano jioni kimeanza rasmi mazoezi kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Mbeya City.

Wachezaji wa kikosi hicho waliokuwa mapumziko kwa siku moja mara baada ya kurejea kutoka mkoani Mwanza juzi Jumatatu, wameanza mazoezi hayo kujiandaa na mtanange huo utakaopigwa Uwanja wa Sokoine, mkoani Mbeya Jumapili hii saa 10.00 jioni.

Nyota wote wamerejea vema mazoezini, ambapo benchi la ufundi limejinasibu ya kuwa watakipanga vema kikosi kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye mchezo huo unaotarajia kuwa wa ushindani mkubwa.

Kikosi hicho kitaendelea tena na mazoezi kesho Alhamisi na Ijumaa muda ule ule wa jioni, kabla ya Jumamosi kuanza safari ya kueleka mkoani Mbeya kwa ndege, tayari kumalizia mchezo wa mwisho msimu huu ndani ya jiji la Mbeya.

Timu hizo zilipokutana kwenye raundi ya kwanza, Azam FC ilishinda mabao 2-0, yaliyofungwa na kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu na mshambuliaji Danny Lyanga, ukiwa ni mchezo uliofungua pazia la msimu huu kwa timu hiyo.