MSHAMBULIAJI wa Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati Azam FC, Mbaraka Yusuph, anatarajia kukaa nje ya dimba kwa muda wa miezi tisa ijayo baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti jijini Cape Town, Afrika Kusini jana.

Nyota huyo amekutwa na tatizo la kuchanika mtulinga wa kati wa goti lake la mguu wa kulia (Anterior Cruciate Ligament Tear), hali iliyolazimika afanyiwe upasuaji huo.

Yusuph aliyepata majeraha hayo wakati akiwa kwenye kikosi cha Namungo kinachoshiriki Ligi Daraja la Kwanza (FDL), iliyomchukua kwa mkopo hadi mwisho wa msimu huu, amefanyiwa upasuaji huo katika Hospitali ya Vincent Pallotti iliyopo nchini humo.

Daktari wa Azam FC, Dr. Mwanandi Mwankemwa, aliyeongozana na mshambuliaji huyo nchini humo kushughulikia matibabu yake, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz kuwa Yusuph anatarajia kurejea tena dimbani kwa ajili ya ushindani Desemba 8 mwaka huu.

“Upasuaji wa Mbaraka Yusuph umemalizika salama, amefungwa kifaa maalumu cha kulinda goti lake kwa muda wa wiki nne kutoka sasa ‘knee brace’, baada ya hapo kifaa hicho kitafunguliwa na kuanza rasmi mazoezi madogo madogo ya kutibu jeraha lake ‘Physiotherapy’,” alisema.

Alisema baada ya miezi mitatu kupita, mshambuliaji huyo ataruhusiwa kuanza mazoezi ya kukimbia na kuendesha baiskeli atakayofanya hadi miezi tisa kupita atakaporuhusiwa kurejea dimbani kuanza mazoezi ya ushindani na kucheza.

Yusuph alikuwa na kiwango bora tokea ajiunge na kikosi hicho kwa mkopo kwenye usajili uliopita wa dirisha dogo uliomalizika Desemba 15 mwaka jana, akiwa amefunga mabao kadhaa yaliyoiwezesha hadi sasa Namungo ipo kileleni mwa Kundi A katika FDL ikiwa imejikusanyia pointi 37.