KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetoka suluhu dhidi ya Mbao katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo Jumapili.

Matokeo hayo yanaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 63 ikiendelea kubakia nafasi ya pili kwenye msimamo, ikizidiwa pointi tano na Yanga yenye mchezo mmoja mkononi iliyo kileleni ikiwa nazo 68.

Azam FC ilifanikiwa kupata nafasi takribani tatu za wazi za kufunga mabao kipindi cha kwanza, mbili zikipotezwa na mshambuliaji Donald Ngoma na nyingine akiikosa mshambuliaji Obrey Chirwa, aliyeruka kichwa cha kuchumpa kilichotoka pembeni ya lango.

Kipindi cha pili ilijitahidi kusaka mabao zaidi hasa alipoingia winga Joseph Mahundi, ambaye aliongeza kasi ya mashambulizi lakini ilishindwa kutumia vema nafasi ilizopata huku pia mwamuzi wa mchezo huo, Ahmada Simba (Kagera) akionekana kufanya maamuzi mengi tata ya kuwapunguza kasi wachezaji wa timu hiyo.

Dakika ya 90 mwamuzi huyo alimuonyesha kadi nyekundu nahodha wa Azam FC, Agrey Moris, akidai alimkwatua makusudi mshambuliaji wa Mbao, Lukindo, kadi ambayo ilionekana nyepesi kutolewa na mwamuzi huyo.

Sare hiyo inaifanya Azam FC kutoka suluhu ya pili mfululizo dhidi ya Mbao kwenye uwanja huo, ambao haijawahi kushinda dhidi ya timu hiyo na pia ikiwa imepoteza mara moja huku ikishinda mechi zote tatu ilizocheza nayo Azam Complex.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam kesho Jumatatu alfajiri tayari kuanza maandalizi ya kuzikabili, Mbeya City (Aprili 14) na Ndanda (Aprili 18), itakazocheza nazo kwenye mechi zijazo ugenini.

Kikosi cha Azam FC leo:

Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Yakubu Mohammed, Agrey Moris (C), Mudathir Yahya/Salmin Hoza dk 64, Salum Abubakar, Frank Domayo, Donald Ngoma, Obrey Chirwa/Paul Peter dk 81, Danny Lyanga/Joseph Mahundi dk 56