BAADA ya kupata ushindi mfululizo mechi nne za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL), Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kuendeleza makali yake itakapokuwa ikikabiliana na Mbao kwenye Uwanja wa CCM Kirumba kesho Jumapili saa 10.00 jioni.

Mchezo huo unatarajia kuwa mkali na wa aina yake hasa kutokana na fomu nzuri ya matokeo ya hivi karibuni ya Azam FC huku Mbao nao ikitaka kuondoa rekodi ya kufungwa mechi tano mfululizo kwenye ligi hiyo inayoendelea kutimua vumbi.

Kikosi cha Azam FC ambacho kipo mkoani Mwanza kwa wiki moja hivi sasa, kimetoka kuichapa Kagera Sugar mabao 2-0 kwenye mchezo uliopita uliofanyika Uwanja wa Nyamagana, huku Mbao ikipoteza bao 1-0 nyumbani dhidi ya Biashara United katika mtanange wao uliopita.

Benchi la ufundi la Azam FC pamoja na wachezaji, wameshaweka malengo makali ya kuhakikisha inavuna ushindi mfululizo kwenye mechi zote wanazocheza ili kumaliza katika nafasi nzuri, hadi hivi sasa wakiwa wamejikusanyia pointi 62 ikiwa nafasi ya pili wakizidiwa pointi sita na vinara Yanga.

Azam FC inatarajia kuwakosa wachezaji wake wanne kuelekea mchezo huo, kipa Razak Abalora, akiendelea kutumikia adhabu ya kadi nyekundu, huku viungo Stephan Kingue, Tafadzwa Kutinyu na winga Ramadhan Singano, ambao wamesimamishwa kucheza mechi tatu zijazo na Kamati ya Nidhamu ya TFF wakidaiwa kumzonga mwamuzi kwenye mchezo wa Azam FC iliotoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Coastal Union.

Kihistoaria huo utakuwa ni mchezo wa sita kwa timu hizo kukutana Ligi Kuu, mechi tano za awali Azam FC imeshinda mara mbili zote ikiwa Azam Complex, ikapoteza moja na suluhu mbili, zote wakati ikiwa ugenini katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.

Ushindi wowote kwa Azam FC kesho utakuwa ni kihistoria kwa timu hiyo ndani ya uwanja huo dhidi ya Mbao, ambapo kwenye mchezo wa raundi ya kwanza Azam FC ilishinda mabao 4-0, yaliyofungwa na Nahodha Agrey Moris, Joseph Mahundi aliyefunga mawili na kiungo aliyekuwa katika ubora wake, Salum Abubakar ‘Sure Boy’.

Mara baada ya mchezo huo kikosi cha Azam FC kinatarajia kurejea jijini Dar es Salaam, tayari kuanza maandalizi ya mechi mbili nyingine za ugenini dhidi ya Mbeya City (Aprili 14) na Ndanda (Aprili 18) kabla ya kuvaana na Yanga Aprili 29 na kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Fedeation Cup) dhidi ya KMC.