NAHODHA msaidizi wa Azam FC, Frank Domayo ‘Chumvi’, ameeleza siri ya kufunga mabao ya mashuti ya mbali akidai kuwa ni mazoezi na jitihada binafsi.

Domayo ambaye ametoka kwenye majaraha ya muda mrefu ya goti yaliyomweka nje ya dimba kwa miezi minne hadi aliporejea katikati ya mwezi Februari, juzi alifunga bao lake pili wakati Azam FC ikiichapa Kagera Sugar 2-0, lingine alifunga kwa staili ile ile aliporejea kwa mara kwanza dimbani, timu yake ilipopoteza 3-1 dhidi ya Simba.

“Kwanza kabisa lazima ufanye mazoezi mwenyewe binafsi ‘individual’, kwa sababu unakumbuka mimi nilikuwa nje kwa muda mrefu kwa hiyo lazima ufanye mazoezi uwe vizuri ili uweze kuwa sawa na wenzako ‘copy’.

“Kwa hiyo naweza kusema Mungu pia alikuwa upande wangu kwa sababu unaweza ukapiga shuti ukakosa, unaweza ukapiga shuti ukapata…ni jitihada binafsi za kufanya mazoezi na pia nawashukuru Azam kwa kunipeleka kwenye kituo bora kabisa cha mazoezi ambacho walikuwa wananipa programu nzuri na ndio maana nimerudi vizuri,” alisema Domayo wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz

Kiungo huyo mwenye uwezo wa kukaba na kupandisha mashambulizi mbele, alisema kuwa watahakikisha wanapambana ili kuweza kupata pointi zingine tatu kwenye mchezo ujao wa ligi dhidi ya Mbao, unaotarajia kufanyika Uwanja wa CCM Kirumba Jumapili ijayo saa 10.00 jioni.

“Mbao ni timu nzuri na sisi pia ni timu nzuri, tutakaa na makocha vizuri watatupa mbinu, tukifata mbinu za kocha siku zote inakuwa ni ushindi kwetu kwa sababu makocha ndio wanajua udhaifu na ubora wa timu,” alisema.

Kuelekea mchezo huo, kikosi cha Azam FC kimeanza rasmi mazoezi leo jioni baada ya mapumziko ya siku ya jana, wachezaji wameonekana kuanza mazoezi isipokuwa mshambuliaji Obrey Chirwa, ambaye amepumzishwa.

Azam FC hadi sasa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikiwa na pointi 62 ikizidiwa pointi nane na vinara Yanga waliokuwa nazo 68 huku Simba iliyonafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 22 ikiwa nazo 57.