TIMU ya vijana ya Azam FC (Azam U-20) imefanya kweli usiku huu baada ya kuitandika Yanga U-20 kwa mikwaju ya penalti 7-6 na kutwaa ubingwa wa michuano ya vijana ya JMK (JMK Youth Tournament).

Mpambano huo uliokuwa mkali na wa aina yake ulilazimika kufika hatua ya kupigiana matuta baada ya kumalizika kwa sare ya bao 1-1 katika muda wa kawaida wa mchezo.

Azam U-20 ndio iliyokuwa ya kwanza kuziona nyavu za wapinzani wake, kupitia kwa bao safi la Hamis Ngoengo dakika ya 37 kabla ya Eric Msagati, kuisawazishia Yanga dakika ya 70 na kufanya mpira kwenda hatua ya matuta.

Waliofunga penalti saba zilizoipa ubingwa Azam U-20 ni Emmanuel Kabelege, Abdallah Mkulu, Abadi Kawambwa, Samwel Onditi, Steven Aduah, Ashraf Said na kipa Wilbol Maseke.

Timu hizo zilikutana pia kwenye hatua ya makundi na kutoka sare ya bao 1-1, zote zikitoka Kundi B na kutengeneza mchezo mkali wa fainali uliuhudhuriwa na mashabiki wengi.

Kabla ya kufika fainali, Azam U-20 ilianza vema hatua ya makundi kwa kuzichapa African Lyon (5-0), JKT Tanzania (6-1) kabla ya kutoka sare na Yanga kwenye mchezo wa mwisho wa hatua hiyo.

Azam U-20 ikapenya hadi nusu fainali ikiwa kinara wa kundi kwa pointi saba, ambapo kwenye hatua hiyo ilikutana na wenyeji JMK na kuwachapa 2-0 na kutinga fainali ilipofanikiwa kutwaa taji hilo.

Tuzo binafsi za michuano:

Michuano hiyo haijaisha hivi hivi, kwani waandaji waliweza kuwatunuku wachezaji waliofanya vizuri, ambapo Tuzo ya Mchezaji Bora wa michuano ilienda kwa nahodha wa Azam U-20, Samuel Onditi.

Kipa wa Azam U-20, Wilbol Maseke, akazoa tena Tuzo ya Kipa Bora, mshambuliaji wa Yanga, Erick Msagati, amenyakua Tuzo ya Ufungaji Bora kwa mabao yake saba aliyofunga, huku Kocha aliyesimamia kikosi cha Azam kwenye michuano hiyo, John Matambara, akibeba Tuzo ya Kocha Bora.

Matambara ameshika kwa muda mikoba ya Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ambaye ameambatana na timu kubwa ya Azam FC, iliyopo mkoani Mwanza kucheza mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) akiwa sehemu ya benchi la ufundi la timu hiyo hivi sasa.