KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imezidi kunawiri kwenye mechi ya pili mfululizo dhidi ya Kagera Sugar baada ya kuichapa mabao 2-0, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) uliofanyika Uwanja wa Nyamagana, Mwanza.

Itakumbukwa kuwa kabla ya timu hizo kukutana leo Jumanne, zilitifuana Ijumaa iliyopita kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), Azam ikishinda bao 1-0.

Lakini kiujumla huo ni mchezo wa tatu msimu huu kukutana, Azam FC ikiwa imeshinda mara zote, ambapo kabla ya mechi hizo mbili za karibuni, zilianzia kwenye raundi ya kwanza ya ligi, mabingwa hao wakishinda 1-0 kwenye Uwanja wa Kaitaba.

Ushindi wa leo kwenye ligi, unaifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 62 ikiwa nafasi ya pili katika msimamo wa ligi, ikizidiwa pointi tano na kinara Yanga iliyokuwa nazo 67 lakini ikiwa na mchezo mmoja mkononi, Simba iliyocheza mechi 22 ipo nafasi ya tatu ikijikusanyia 57.

Azam FC ilianza mchezo huo kwa kasi na kujipatia bao la uongozi dakika ya nne tu ya mchezo, lililofungwa kwa shuti kali nje ya eneo la 18 na nahodha msaidizi, Frank Domayo ‘Chumvi’, akimalizia pasi safi ya mkato ya beki wa kushoto, Nickolas Wadada.

Mabingwa hao wa ligi msimu 2013/2014 waliimarisha zaidi ushindi wao huo. kwa kujipatia bao la pili dakika 85 kupitia kwa mshambuliaji Donald Ngoma, akifunga kwa niia ya mkwaju wa penalti kufuatia Danny Lyanga, kuangushwa ndani ya eneo la hatari na kipa, Jeremiah Kisubi, na mwamuzi Erick Onoka kutoka Arusha kuamuru adhabu hiyo.

Hilo ni bao la 10 kwa Ngoma kwenye msimu huu wa ligi, akiwa anamfukuzia mshambuliaji Salum Aiyee wa Mwadui aliye kileleni katika chati ya ufungaji bora kwa mabao yake 16, lakini hadi sasa akiwa ndio mfungaji bora wa matajiri kutoka viunga vya Azam Complex.

Huo unakuwa ushindi wa sita mfululizo kwa kikosi cha Azam FC, ikiwa chini ya makocha wa muda, Idd Nassor Cheche na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ambao wamechukua timu hiyo mara baada ya kufukuzwa na Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi.

Walianza kwa kuichapa Rhino Rangers mabao 3-0 kwenye hatua ya 16 bora ya Kombe la FA, ikazinyuka tena African Lyon (3-1), JKT Tanzania (6-1), Singida United (4-0), Kagera Sugar (1-0) ikiwa ni ya FA na kabla ya leo kuinyuka tena Kagera (2-0) katika ligi.

Mara baada ya mchezo huo, Azam FC itaendelea kusalia tena mkoani Mwanza, ikitarajia kukipiga dhidi ya Mbao Jumapili hii, mechi itakayopigwa Uwanja wa CCM Kirumba, saa 10.00 jioni.

Kikosi cha Azam FC leo:

Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda/Yakubu Mohammed dk 46, Agrey Moris (C), Salmin Hoza, Joseph Mahundi/Idd Kipagwile dk 87, Frank Domayo, Donald Ngoma, Obrey Chirwa/Danny Lyanga dk 72, Salum Abubakar