TIMU ya vijana ya Azam FC (Azam U-20) imetinga fainali ya michuano ya vijana ya JMK (JMK Youth Tournament) baada ya kuwachapa wenyeji JMK mabao 2-0 usiku wa jana Jumatatu.

Azam U-20 imekuwa na muendelezo wa kiwango kizuri kwenye michuano hiyo, na sasa kwenye fainali itakutana na Yanga itakayofanyia Uwanja wa JMK keshokutwa Alhamisi saa 12.00 jioni.

Fainali hiyo itakumbushia mechi ya hatua ya makundi, timu hizo zilizokuwa Kundi B, na zilipokutana zilitoka sare ya bao 1-1, bao la Azam U-20 likifungwa kwa mkwaju wa penalti na Nahodha, Samuel Onditi.

Vijana hao wa Azam wametinga fainali kwa kupata ushindi huo dhidi ya JMK, kupitia kwa mabao ya winga Emmanuel Kaberege aliyetupia la kwanza dakika ya 39 huku jingine likiwekwa kimiani dakika ya 65 na Onditi, kwa mkwaju wa penalti iliyotokana na mshambuliaji wa Azam U-20, Hamisi Ngoengo, kuangushwa kwenye eneo la 18.

Azam U-20, ilifuzu hatua ya nusu fainali baada ya kushinda mechi mbili za makundi, ikizichapa African Lyon (5-0), JKT Tanzania (6-2) kabla ya kutoka sare na Yanga.