KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kimewasili salama mkoani Mwanza leo Jumamosi saa 9 Alasiri huku Kocha Idd Nassor Cheche, akitamba kuwa watafanya kitu kikubwa zaidi dhidi ya Kagera Sugar.

Azam FC imewasili mkoani humo ikitokea mkoani Kagera ilipoichapa Kagera Sugar bao 1-0 jana na kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup), bao lililofungwa kiustadi na winga Joseph Mahundi.

Ikiwa mkoani Mwanza, Azam FC itarudiana tena na Kagera Sugar, safari hii ikiwa ni mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) itakayofanyika Uwanja wa Nyamagana, Aprili 3 mwaka huu.

Matajiri hao wanatarajia kuwa wenyeji kwenye mchezo huo, na wanautumia uwanja huo baada ya ule wa Azam Complex kufungwa kupisha maandalizi ya fainali ya Mataifa ya Afrika kwa Vijana chini ya umri wa miaka 17 (AFCON U-17), Tanzania ikiwa mwenyeji wa michuano hiyo itakayoanza kutimua vumbi kuanzia Aprili 14 hadi 28 mwaka huu.

“Mechi ya mtoano ni tofauti na ya ligi, mimi nasema mechi ya ligi (Kagera Sugar) watu watashangaa jinsi matokeo yatakavyokuwa tutaonyesha kitu kikubwa zaidi, maana yake mechi ya ligi huwa haina presha kama hii (Kombe la FA) kwa sababu kila mtu anakuwa na wasiwasi hasa ukipigwa goli, lakini kwenye ligi tutaonyesha mambo makubwa mpaka watu watashangaa,” alisema Cheche wakati akizungumza na mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz  

Mbali na kucheza na Kagera Sugar, mabingwa hao wa ligi msimu wa 2013/2014 wanatarajia kuwa ugenini kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, itakapokipiga dhidi ya Mbao Aprili 8 mwaka huu.