KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imetinga nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) baada ya kuichapa Kagera Sugar bao 1-0, mchezo uliofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera.

Ushindi huo muhimu unaifanya Azam FC kukutana KMC katika hatua hiyo, mchezo unaotarajia kupigwa Uwanja wa Azam Complex mwezi Mei mwaka huu, ambapo wapinzani wao hao wametinga nusu fainali baada ya kuichapa African Lyon mabao 2-0.

Azam FC ililazimika kusubiri hadi dakika ya 79 kuweza kujipatia bao hilo la ushindi lililofungwa kiustadi na winga Joseph Mahundi, aliyetumia vema pasi ya mpenyezo ya kiungo mkabaji, Stephan Kingue.

Mechi hiyo ilikuwa na ushindani mkubwa, ambapo Azam FC ilijitahidi kufanya majaribio kadhaa kupitia kwa washambuliaji wake, Donald Ngoma, Obrey Chirwa na kiungo Mudathir Yahya kabla ya kupata bao hilo.

Azam FC ililazimika kucheza pungufu dakika 23 za mwisho za mchezo huo, baada ya kipa Razak Abalora, kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Shomari Lawi, baada ya kumfanyia madhambi mchezaji wa Kagera Sugar aliyekuwa akienda kufunga bao.

Baada ya kadi hiyo nhyekundu, benchi la ufundi la Azam FC lililazimika kumfanyia mabadiliko mshambuliaji Obrey Chirwa na kumwingiza kipa Mwadini Ally, ili akazibe pengo hilo la Abalora.

Mara baada ya mchezo huo kikosi cha Azam FC kinatarajia kuelekea mkoani Mwanza kesho Jumamosi asubuhi tayari kukipiga tena na Kagera Sugar kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) utakaopigwa Uwanja wa Nyamagana Aprili 3 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC leo:  

Razak Abalora (Red Card dk 69), Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, Lusajo Mwaikenda, Agrey Moris (C), Stephan Kingue, Joseph Mahundi, Mudathir Yahya/Frank Domayo dk 63, Donald Ngoma, Obrey Chirwa/Mwadini Ally dk 69, Ramadhan Singano/Enock Atta