KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, inatarajia kusaka nafasi ya kuingia hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) kwa kupambana na Kagera Sugar, mchezo utakaopigwa Uwanja wa Kaitaba kesho Ijumaa saa 10.00 jioni.

Azam FC inauchukulia kwa uzito mkubwa mchezo huo, kutokana na kiu yake kubwa ya kutwaa taji la michuano hiyo na kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, baada ya kukosa michuano ya Afrika kwa miaka miwili.

Kikosi cha timu hiyo tayari kimewasili mjini Bukoba, Kagera tokea juzi kikiwa na ari kubwa ya kusaka ushindi, ambapo jana asubuhi kilifanya mazoezi ya kwanza mjini humo huku jioni ya leo kikitarajia kufanya maandalizi ya mwisho kabla ya kuvaana na Kagera Sugar.

Wachezaji wote wapo fiti kabisa kwa mchezo huo, isipokuwa beki David Mwantika, ambaye ana maumivu ya mguu huku kiungo mshambhuliaji Tafadzwa Kutinyu, akiwa bado hajaungana na kikosi cha timu hiyo baada ya kuwa kwenye majukumu ya timu yake ya Taifa ya Zimbabwe,

Kuelekea mchezo huo, Kocha wa timu hiyo, Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ambaye yuko sambamba na Idd Nassor Cheche, alisema kuwa morali iko juu kikosini, huku akitamba wachezaji wote wanataka kubeba kikombe cha michuano hiyo.

“Tumecheza michezo minne tukapata matokeo, wachezaji wote morali ipo juu na wao wanataka kabisa hiki kikombe cha FA tukichukue, kwa hiyo tumetilia mkazo kuanzia walimu, uongozi pamoja na wachezaji,” alisema.

Huo ni mchezo wa kwanza kwa timu hizo kukutana kwenye michuano hiyo, lakini utakuwa ni mchezo wa 22 wa mashindano kupambana, Azam FC ikiwa na uwiano mzuri wa kushinda ambapo katika mechi 21 zilizopita, imeshinda mara 11, ikapoteza mara tano huku ikipata sare tano.

Mara ya mwisho timu hizo kukutana msimu huu, Azam FC ilishinda bao 1-0 ukiwa ni mchezo wa ligi uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, bao la matajiri hao likiwekwa kimiani na mshambuliaji aliyekuwa katika fomu ya aina yake, Donald Ngoma, aliyeunganisha pasi ya Kutinyu.

Aidha kama Azam FC ikifanikiwa kumtoa Kagera Sugar, itakata tiketi ya nusu fainali na kukutana na KMC, ambayo jana iliilaza African Lyon mabao 2-0, mchezo wa robo fainali uliopigwa kwenye Uwanja wa Meja Isamuhyo.

Mara ya kwanza Azam FC kutinga fainali ya michuano hiyo ilikuwa ni msimu 2015/2016, ikipoteza dhidi ya Yanga kwa kufungwa mabao 3-1, bao la matajiri hao likiwekwa kimiani na aliyekuwa mshambuliaji wa timu hiyo, Didier Kavumbagu.