TIMU ya vijana ya Azam FC (Azam U-20) imezidi kuchanua kwenye michuano ya vijana ya JMK Park baada ya kuitandika JKT Tanzania U-20 6-2, mchezo uliofanyika Uwanja wa JMK Park juzi.

Huo ni ushindi wa pili mfululizo kwa Azam U-20 kwenye michuano hiyo, baada ya mchezo wa kwanza kuinyuka African Lyon mabao 5-0 huku ikishuhudiwa mshambuliaji Paul Peter, akifunga hat-trick yaani mabao matatu kwenye mtanange huo.

Azam U-20 ilijipatia mabao yake dhidi ya maafande hao, kupitia kwa mshambuliaji Abadi Kawambwa, nahodha Samuel Onditi, John Mpundunga, Bakari Bilali, Emmanuel Kibelege na Ashraf aliyetupia la mwisho.

Ushindi huo unaifanya timu hiyo kuendelea kusalia kileleni mwa msimamo wa Kundi B la michuano hiyo ikiwa na pointi sita na mabao 11 ya kufunga kwenye mechi mbili tu ilizocheza, ikifuatiwa na Yanga U-20 yenye pointi nne, JKT Tanzania iliyojikusanyia moja huku Lyon ikiburuza mkia ikiwa haina pointi.

Wababe hao wanatarajia kumalizia hatua ya makundi kwa kumenyana na Yanga U-20, mchezo utakaofanyika Uwanja wa JMK Park Ijumaa hii saa 2.00 usiku, utakaotanguliwa na mtanange kati ya African Lyon na JKT Tanzania utakaoanza saa 12.00 jioni.