IKIWA inajiandaa kuelekea mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Kagera Sugar, Azam FC imeichapa Buyuni FC mabao 6-0 kwenye mchezo wa kirafiki uliofanyika Uwanja wa Azam Complex leo Jumamosi asubuhi.

Mchezo huo ulikuwa ni maalumu kwa ajili ya benchi la ufundi kuwaweka kwenye ushindani wachezaji na kuwapima kabla ya kuelekea katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar, utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Kagera Machi 29 mwaka huu saa 10.00 jioni.

Mabao ya Azam FC yamefungwa na winga Joseph Mahundi, ambaye alikuwa akicheza kama beki wa kulia, mshambuliaji Donald Ngoma, Paul Peter huku Danny Lyanga, aliyecheza dakika zote 90 akifunga mabao matatu yaani ‘hat-trick’.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC kinatarajia kupumzika kesho Jumapili kabla ya kuanza safari ya kuelekea mkoani Kagera keshokutwa Jumatatu alfajiri, tayari kuonyeshana kazi na Kagera Sugar, katika mchezo unaotarajiwa kuwa mkali na wa aina yake.

Wachezaji wote wa Azam FC wapo fiti na kamili kwa ajili ya kufanikisha timu hiyo kutinga nusu fainali ya michuano hiyo na hatimaye kuingia fainali na kutwaa taji hilo, litakaloifanya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.