TIMU ya vijana ya Azam FC chini ya umri wa miaka 20 (Azam U-20) inatarajia kushirikia michuano ya JMK U-20 kwa kukipiga dhidi ya African Lyon mchezo utakaopigwa Uwanja wa JMK Park kesho Ijumaa, saa 2.00 usiku.

Michuano hiyo iliyoanzishwa na Kituo cha JMK Park kilichopo Kidongo Chekundu, jijini Dar es Salaam, inatarajia kushirikisha jumla ya timu nane ikifanyika kwa muda wa wiki mbili ikiwa imeanza rasmi leo Alhamisi.

Miongoni mwa timu shiriki ukiondoa Azam U-20, ni wenyeji JMK Park, Yanga, KMC, JKT Tanzania, African Lyon, JKU ya Zanzibar na Navy Kenzo, ikiwa ni timu inayomilikiwa na moja ya wasanii maarufu nchini, Nahreel.

Mechi mbili zilizofungua pazia la michuano hiyo leo Alhamisi, ni KMC waliotoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya JKU huku wenyeji JMK wakiichapa Navy Kenzo 2-0, mchezo uliomalizika usiku huu.

Kikosi cha Azam U-20 kipo kamili kwa ajili ya michuano hiyo na kimejiandaa vilivyo kutwaa taji kikiwa kinanolewa na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ambaye pia ni kocha wa muda wa timu kubwa ya Azam FC akiwa sambamba na Idd Nassor Cheche, ambao wamekiongoza vema kikosi cha matajiri hao kwenye mechi nne zilizopita.

Mbali na mchezo wa Azam U-20 kesho, mchezo wa utangulizi utakaoanza saa 12.00 jioni, utawahusisha timu ya vijana ya Yanga watakaopiga na JKT Tanzania, mechi zote zikipigwa ndani ya dimba la JMK Park.