WAKATI kikosi cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kikitarajia kuanza mazoezi leo Jumanne jioni kujiandaa na mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Kagera Sugar, tayari wachezaji wanne wamejiunga kwenye kambi ya timu zao za Taifa.

Mchezo huo wa robo fainali, utafanyika Uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera Machi 29 mwaka huu, ambapo Azam FC inauchukulia kwa uzito mkubwa mtanange huo ili kutimiza lengo la kushiriki michuano ya Afrika msimu ujao.

Wachezaji wa Azam FC watakaokosekana kwenye mazoezi ya leo baada ya kuripoti timu zao za Taifa kumalizia mechi za mwisho za kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika mwaka huu nchini Misri, ni nahodha Agrey Moris, kiungo mkabaji Mudathir Yahya (Tanzania), beki wa kushoto Nickolas Wadada (Uganda) na kiungo mshambuliaji Tafadzwa Kutinyu (Zimbabwe).

Kikosi cha Azam FC kimekuwa na mwenendo mzuri hivi sasa  baada ya kuwa chini ya makocha wa muda, Idd Nassor Cheche na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ambao wameiongoza timu hiyo kushinda mechi nne mfululizo kwa ushindi mnono, jambo ambalo limewafanya wakubalike na mashabiki wa timu hiyo.

Katika mechi nne walizoshinda, wamewapasua Rhino Rangers (3-0) na kutinga robo fainali ya ASFC na mechi za ligi zilizofuata ilizinyuka African Lyon (3-1), JKT Tanzania (6-1) na Singida United (4-0).

Cheche, ameshaweka wazi kuwa anawasubiria mazoezini leo nyota wake, ili kuweza kuwapa mbinu na mazoezi tayari kwa mapambano ya mchezo huo, huku akisema ni mapema mno kuuzungumzia mchezo huo japo amekiri mechi za mashindano hayo ni kama fainali kwao.

Aidha kwa kuonyesha wamedhamiria kutinga nusu fainali ya michuano hiyo na hatimaye fainali na kubeba taji, kikosi kazi cha Azam FC kinatarajia kuondoka jijini Dar es Salaam kuelekea mjini Bukoba, Kagera Jumatatu ijayo (Machi 25) alfajiri, ikiwa ni safari ya siku mbili kabla ya kuwasili tayari kupambana na Kagera Sugar.

Bingwa wa michuano hiyo anatarajia kuiwakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao, mbali na kubeba kikombe na medali za dhahabu, pia bingwa atajinyakulia kitita cha Sh. milioni 50.