KLABU Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, imeendeleza dozi nene baada ya kuichapa Singida United mabao 4-0.

Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) umefanyika Uwanja wa Azam Complex, ushindi huo umeifanya Azam FC kufikisha jumla ya pointi 62 katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi ikizidiwa pointi nane na Yanga iliyo kileleni kwa pointi 70.

Matajiri hao kabla ya kuongeza ushindi huo mnono, walitoka kuichapa JKT Tanzania mabao 6-1 kwenye mchezo uliopita, ukiwa ni ushindi mnono zaidi msimu huu.

Singida iliyokuwa ikipoteza muda mara kadhaa kipindi cha kwanza kwa wachezaji wake kujidondosha mara kwa mara, iliweza kufanikiwa kuibana Azam FC isifunge bao kipindi cha kwanza.

Beki wa Azam FC, David Mwantika, alilazimika kufanyiwa mabadiliko dakika ya 35 baada ya kupata majeraha, na nafasi yake ilichukuliwa na Lusajo Mwaikenda, ambaye ni nahodha wa timu ya vijana ya mabingwa hao (Azam U-20), aliyeonekana kuziba vema pengo lake.

Winga Ramadhan Singano, alifanikiwa kuipatia bao la uongozi dakika ya 66 baada ya shuti alilopiga kumbabatiza beki na mpira kumshinda kipa wa Singida United, Said Lubawa, na kujaa kimiani, pasi ya kiungo Salmin Hoza.

Dakika ya 73, Mahundi alipigilia msumari wa pili kwa shuti zuri akimalizia pasi ya kichwa mshambuliaji Obrey Chirwa, likiwa ni bao lake sita kwenye ligi msimu huu.

Mshambuliaji Donald Ngoma, aliyeingia dakika ya 42 kuchukua nafasi ya Tafadzwa Kutinyu, alihitimisha ushindi mnono wa Azam FC kwa kufunga mabao mawili ya mwisho, la kwanza akifunga dakika ya 76 baada ya kuunasa mpira uliotokana na shuti na Enock Atta kuwababatiza mabeki, huku jingine akitupia dakika ya 89 akitumia vema pasi ya Chirwa.

Ngoma kwa kufunga mabao hayo, hivi sasa amesogea kwenye msimamo wa wafungaji bora wa kwenye ligi hiyo, akiwa na mabao tisa, akiwa amezidiwa mabao matano na kinara anayeongoeza Salim Aiyee, kutoka Mwadui aliyefunga matano.

Dakika ya 85 Azam FC ilikosa mkwaju wa penalti, uliopigwa na Enock Atta, baada ya kipa kupangua, nafasi hiyo ya penalti ilitokana na Chirwa kuangushwa kwenye eneo la hatari.

Mara baada ya ushindi huo, kikosi cha Azam FC hivi sasa kinahamishia vita yake kwenye mchezo wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Kagera Sugar utakaofanyika Uwanja wa Kaitaba, mkoani Kagera Machi 29 mwaka huu.

Kikosi cha Azam FC:

Mwadini Ally, Nickolas Wadada, Bruce Kangwa, David Mwantika/Lusajo Mwaikenda dk 35, Agrey Moris (C), Salmin Hoza, Joseph Mahundi, Frank Domayo, Obrey Chirwa, Tafadzwa Kutinyu/Donald Ngoma dk 42, Ramadhan Singano/Enock Atta dk 75