KIKOSI cha Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC, kipo vizuri kabisa kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) dhidi ya Singida United, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex kesho Ijumaa saa 1.00 usiku.

Azam FC inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na morali ya hali ya juu baada ya kutoka kuichapa JKT Tanzania mabao 6-1 huku wapinzani wao Singida wakitoka kupoteza bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar juzi Jumanne.

Wachezaji wako kwenye hali nzuri kabisa tayari kwa mchezo huo, wakionekana kufurahia mazoezi wanayopewa na makocha wapya wa muda, Idd Nassor Cheche na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ambao wameiongoza timu hiyo kushinda mechi tatu mfululizo kwa ushindi mnono.

Kuelekea mchezo huo, Kocha Cheche amesema kuwa wamepanga kuendeleza mazuri waliyoonyesha kwenye mechi zilizopita huku akiwapongeza wachezaji kwa kazi nzuri wanayoendelea kufanya mazoezini na katika mechi wanazocheza.

“Mechi ya JKT Tanzania imeshakwisha, macho na akili zetu tunazielekeza katika mchezo wetu wa kesho dhidi ya Singida United, wapinzani wetu ni wazuri sana, tumeshajua ubora na udhaifu waliokuwa nao, vyote tumeshavifanyia kazi,” alisema.

Azam FC itawakosa viungo wake wakabaji wawili kwenye mchezo huo, Mudathir Yahya na Stephan Kingue, ambao watakuwa wakitumikia adhabu ya kukosa mechi moja kila mmoja baada ya kukusanya kadi tatu za njano, lakini hilo haliwaumizi kichwa benchi la ufundi, kwani wameweka wazi kuwa wana wachezaji wazuri wa kuziba nafasi hizo.

Pia itamkosa kiungo mshambuliaji, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, ambaye anasumbuliwa majeraha ya kigimbi cha mguu baada ya kuumia kwenye mchezo uliopita dhidi ya JKT Tanzania.

Mchezo huo utakuwa ni wa tano kihistoria kwa Azam FC kukutana na Singida United kwenye michuano mbalimbali na mara ya nne katika ligi, matajiri hao kutoka viunga vya Azam Complex wakiwa wameshinda mara tatu na mechi moja wakienda sare.

Aidha katika mchezo wa mwisho uliofanyika raundi ya kwanza, Azam FC ilishinda ugenini bao 1-0 lililofungwa na mshambuliaji Donald Ngoma, akiunganisha pasi ya Yahya Zayd, aliyetimkia Ismaily ya Misri.

Hadi sasa kikosi cha Azam FC kikiwa kimeshacheza mechi 28 za ligi, kimejikusanyia jumla ya pointi 59 katika nafasi ya pili kwenye msimamo, kikizidiwa pointi 11 na Yanga, aliyejikusanyia 70 kileleni huku Simba iliyocheza mechi 20 ikiwa nafasi ya tatu baada ya kujizolea 51.