MCHEZO wa Ligi Kuu Tanzania Bara (TPL) kati ya Klabu Bingwa ya Afrika Mashariki na Kati, Azam FC na Singida United, uliokuwa ufanyike Jumamosi hii, sasa utapigwa Ijumaa hii kwenye Uwanja wa Azam Complex saa 1.00 usiku.

Bodi ya Ligi Kuu Tanzania Bara (TPLB), imefanya mabadiliko hayo kutokana na mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika, kati ya Simba na AS Vita ya Congo kufanyika Jumamosi hii kwenye muda sawa na ule ambao mechi ya Azam FC dhidi ya Singida ingefanyika.

Katika kujiandaa vilivyo na mchezo huo, kikosi cha Azam FC kitaanza rasmi mazoezi leo Jumatatu usiku kwa ajili ya kujiweka sawa baada ya kutoka kuichapa JKT Tanzania mabao 6-1 Ijumaa iliyopita.

Kikosi cha Azam FC kipo kwenye mwenendo mzuri hivi sasa baada ya timu hiyo kushikwa na makocha wazawa, Idd Nassor Cheche na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ambao wanafundisha kwa muda wakitoka katika timu za vijana za matajiri hao.

Tokea wakabidhiwe mikoba hiyo baada ya kufukuzwa kwa makocha wa awali, Hans Van Der Pluijm na Msaidizi wake, Juma Mwambusi, hawajapoteza mchezo wowote kwenye mechi tatu walizoziongoza Azam FC, wakizichapa Rhino Rangers (3-0), African Lyon (3-1) kwa kuishushia kipigo kizito JKT.