BAADA ya kuichapa JKT Tanzania mabao 6-1, Kocha wa muda wa Azam FC, Idd Nassor Cheche, amesema kuwa timu hiyo ina matokeo mazuri hivi sasa kutokana na kufanikiwa kucheza na akili za wachezaji.

Azam FC imeibuka na ushindi usiku wa jana, ukiwa ni ushindi mnono wa pili wa mabao zaidi ya mabao matano kuwahi kuupata kwenye ligi hiyo, awali iliwahi kuipiga Villa Squad mabao 6-2 msimu wa 2008/2009.

Mabao ya Azam FC jana yamewekwa kimiani na mshambuliaji Donald Ngoma, aliyetupia mawili, nahodha Agrey Moris, Obrey Chirwa, Mudathir Yahya na Danny Lyanga.

Akizungumza mara baada ya mchezo huo, Cheche anayesaidiana na Meja Mstaafu, Abdul Mingange, ameuambia mtandao rasmi wa klabu www.azamfc.co.tz alisema kama ukishindwa kucheza na akili za wachezaji basi unaweza kuwa na wachezaji wazuri lakini ukashindwa kuwatumia.

“Unaweza ukaja na mazoezi mengi lakini ukaja na vitu vingi lakini bila kucheza na akili zao mafanikio yanakuwa ni magumu,” alisema.

Bao sita za JKT Tanzania

Akizungumzia ushindi huo mnono, licha ya ubora wa timu ya JKT Tanzania, ikiwa ngumu kufungika, Cheche alisema kuwa: “Mimi nasema kwenye mpira linawezekana, kama Brazil waliweza kufungwa goli saba kwao, kwanini JKT wasifungwe goli sita?,” alihoji Cheche.

Huo ni ushindi wa tatu mfululizo kwa kikosi hicho kikiwa chini ya makocha hao wa muda, awali ilitangulia kuzichapa Rhino Rangers (3-0) kwenye kombe la FA na kutinga hatua ya robo fainali kabla ya kuinyuka African Lyon 3-1 kwenye mchezo wa ligi.

Mara baada ya mchezo huo kikosi cha Azam FC, kinatarajia kurejea mazoezini keshokutwa Jumatatu, kuanza maandalizi ya kuikabili Singida United, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex, Machi 16 mwaka huu saa 1.00 usiku.